Latest Posts

WALIODAIWA KUMUUA SUPER SAMI WASHINDA RUFAA NA KUACHIWA HURU

Miaka minane baada ya kifo cha mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Super Sami, Josiah Methusela Mzuri, anayefahamika pia kama Super Sami, Mahakama ya Rufani ya Tanzania imefuta hukumu ya kifo iliyokuwa imewatia hatiani John Simon(Kadaso) na Paul Mashauri (Nchimika,Rubembeja, Jam Marshal) baada ya kubaini mapungufu katika ushahidi uliotumika kuwahukumu.

Wawili hao walikuwa wamehukumiwa kunyongwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, kwa kosa la mauaji.

Uamuzi huo umetolewa Septemba 21, 2026 katika shauri la jinai la rufani namba 432/2024 lililokuwa mbele ya jopo la watatu majaji P. M. Kente, P. F. Kihwelo na L. J. Masabo ambapo mahakama hiyo ilikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuifuta hukumu ya Mahakama Kuu na waliokuwa washtakiwa wakiachiwa huru.

Upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili Peter Kibatala kwa niaba ya John Simon na Augustino Michael Ijani kwa niaba ya Paul Mashauri, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Suzana Masule, akisaidiwa na Joseph Mwakafege na Janeth Dioniz.

Kibatala alidai mbele ya Mahakama ya Rufani kuwa ushahidi wa PW3 ulikuwa na matatizo, huku pia akihoji taarifa za mawasiliano ya simu zilizoonyesha marehemu akiendelea kuwasiliana na John Simon baada ya tarehe ambayo mashtaka yalisema mauaji yalitokea.

Katika utetezi wao, John Simon alikana kuhusika na mauaji hayo na kusema marehemu alikuwa rafiki yake ambaye hata aliwahi kuwa mdhamini wake wakati akikabiliwa na kesi nyingine.

Paul Mashauri naye alikanusha kuhusika na kusema wakati wa tukio alikuwa nyumbani Ukerewe. Mahakama ya Rufani ilibaini kuwa utetezi wa ‘alibi’ wa washtakiwa haukuzingatiwa ipasavyo na Mahakama Kuu, hasa kwa sababu tarehe ya tukio ilikuwa muhimu katika mazingira ambayo washtakiwa walidai walikuwa maeneo mengine.

Mahakama ya Rufani pia ilikataa matumizi ya dhana ya “last seen together” dhidi ya John Simon, ikisema haikuthibitishwa bila shaka kwamba alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu kabla ya kifo chake.

Aidha, Mahakama iliona kuwa kulikuwa na mapungufu katika ushahidi wa gari, umiliki wake, tarehe ya mauaji na mlolongo wa ushahidi wa kimazingira. Kwa mtazamo wa Mahakama, katika kesi inayotegemea ushahidi wa kimazingira, kila kiungo muhimu lazima kiungane bila kuacha uwezekano mwingine wa kutokuwa na hatia huku ikisisitiza kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Hatimaye, Mahakama ya Rufani  ilikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuruhusu rufaa hiyo na hukumu ya hatia dhidi ya John Simon na Paul Mashauri ilifutwa, adhabu ya kunyongwa ikaondolewa na Mahakama ikaamuru waachiwe huru mara moja iwapo hawakuwa wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali.

Kifo cha Super Sami kilitikisa mwaka 2018, baada ya taarifa za kutoweka kwake kusambaa. Taarifa za vyombo vya habari za wakati huo zilieleza kuwa aliondoka Mwanza Februari 27, 2018 akielekea Simiyu kwa shughuli za biashara, lakini hakurejea nyumbani.

Familia ilieleza kuwa kabla ya kutoweka, marehemu alimweleza mkewe kuwa angerudi akiwa na mgeni. Baadaye, gari lake aina ya Nissan Patrol lenye namba T 323 BSF lilikutwa limeteketea kwa moto ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Taarifa ya kushtua zaidi ilikuja Machi 14, 2018, baada ya mwili uliokuwa umefungwa kwenye mfuko kuokotwa katika Mto Ndabaka, eneo la Bunda karibu na mpaka wa Mara na Simiyu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara lilithibitisha kuwa mwili huo ulitambuliwa kuwa wa Josiah Methusela, ambaye alikuwa akiishi Mwanza na kumiliki mabasi ya Super Sami. Wakati huo polisi walisema watu wanne walikuwa wamekamatwa huku uchunguzi ukiendelea kubaini waliohusika na mauaji hayo.

Taarifa hizo za mwaka 2018 ziliendelea kuripoti kuwa kifo cha Super Sami kilihusisha mazingira ya kutatanisha, huku gari lake likiwa limechomwa moto na mwili wake kupatikana ukiwa umefungwa kwenye viroba. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania, TABOA, kupitia msemaji wake Mustapha Mwalongo, kiliitaka Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha mauaji hayo na waliohusika. Wakati huo sababu ya kifo haikuwa imewekwa wazi kwa umma.

Katika kesi iliyofuatia, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 15, ukijenga hoja kwamba John Simon, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa marehemu, alikuwa na deni kwake na kwamba wawili hao walitarajiwa kwenda Kashishi-Karago kwa ajili ya uuzaji wa nyumba. Mashtaka yalidai pia kuwa John Simon alihusisha Paul Mashauri katika mpango huo na kumwahidi malipo ya shilingi milioni tano kwa kazi maalumu, ambayo baadaye ilidaiwa kuwa ni kumuua marehemu.

Shahidi muhimu katika kesi hiyo alikuwa Nelson Charles Rweyemamu, PW3, ambaye alidai kwamba aliajiriwa na John Simon kuendesha gari lililodaiwa kuwa la marehemu kutoka eneo la tukio hadi sehemu ambako mwili ulitupwa. PW3 pia alidai kuwa John Simon alikuwepo pamoja na mtu mwingine na kwamba Paul Mashauri alikuwa akisafiri kwa pikipiki. Hata hivyo, Mahakama ya Rufani baadaye ilibaini kuwa PW3 alikuwa miongoni mwa watu waliowahi kukamatwa kama washukiwa wa kesi hiyo na baadaye akaachiliwa kwa Nolle Prosequi, hivyo ushahidi wake ulipaswa kuchukuliwa kwa tahadhari na kuthibitishwa na ushahidi huru

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!