Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, inaendelea leo Septemba 23, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo Lissu ameanza kuwasilisha majumuisho yake ya mwisho mbele ya jopo la majaji watatu.
Akiwasilisha mahakamani, Lissu ameeleza kuwa kwa sheria za Tanzania na kwa ushahidi uliowasilishwa, haiwezekani kisheria kumhukumu adhabu ya kifo kiongozi wa kisiasa au mwananchi yeyote kwa kutoa maneno ya kisiasa katika mkutano wa kisiasa.
Lissu ameeleza kuhusu mashtaka ya uhaini yanayomkabili akisema kuwa imeelezwa akiwa na utiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 3 Aprili 2025 katika Wilaya ya Kinondoni, alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali. Inadaiwa kuwa alidhihirisha nia hiyo kwa kutamka na kuchapisha maneno haya, “Wanasema kitu kimoja sahihi hapa… msimamo huu unaashiria uasi… tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi… tunaenda kukinukisha… huu uchaguzi tutauvuruga… kwasababu tunaenda kukinukisha vibaya sana.”.
Amesema kwa kuangalia namna maneno hayo yalivyowekwa, kuna mianyo (ellipsis) ambayo inaashiria kuna baadhi ya maneno yaliondolewa.
Wakati wa usikilizaji wa awali tarehe 22 Septemba 2025, Lissu amesema kuwa Jamhuri iliongeza madai kuwa yeye ndiye aliyeitisha mkutano wa watiania, akawaalika waandishi wa habari kutoka Mwananchi, Jambo TV, na Clouds Media, na kwamba kauli zake ziliwachochea baadhi ya wananchi.
Katika majumuisho yake, Lissu ameeleza kuwa hajawahi kukanusha au kuficha maneno yake. Amebainisha kuwa tangu alipokuwa Mahakama ya Kisutu (ukurasa wa 97 wa rekodi za mahakama), alikiri wazi kutamka maneno hayo katika mikutano ya wazi jijini Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Lindi, na Mtwara. Hoja ya msingi si kama alisema maneno hayo, bali ni kama maneno hayo yanatengeneza kosa la uhaini au kosa lolote la jinai kisheria.
Lissu amesisitiza kuwa hana haya wala aibu kwa kauli zake, kwani alichokisema si uhaini na wala si kosa la jinai chini ya sheria za Tanzania.
Ameongeza kuwa baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi 17 wa Jamhuri, kupitia vielelezo 16 vya utetezi, na kutazama ukweli kuwa Jamhuri haikuleta kielelezo hata kimoja cha mashtaka (ikiwemo video yenyewe), kesi ya mashtaka imekuwa dhaifu mno kuliko siku ilipoletwa Mahakama Kuu.
Lissu ameyachambua matakwa ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu na Kifungu cha 10(2) cha sheria hiyo, akibainisha vigezo sita vinavyopaswa kuthibitishwa ili kosa la uhaini liweze kuwepo. Kwanza ni Utiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Pili, ni tendo kufanyika ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano; Tatu ni kutengenezwa kwa nia mahususi ya kutenda kosa la uhaini (si nia ya kufanya jambo jingine); Nne, ni ikiwa ni uchochezi, lazima ulenge mtu mmoja au kikundi cha watu waliotajwa, na si “umma” kwa ujumla; Tano, ni lazima idhihirishwe kwa kuchapisha maandishi au machapisho rasmi; Sita, ni sharti la Kifungu cha 10(2) ambacho ni matokeo halisi kwamba ni lazima kuwe na matokeo halisi yaliyojitokeza kutokana na nia hiyo au uchochezi huo.
Lissu amesisitiza kuwa ikiwa nia ilikuwepo lakini hakuna kosa au matokeo ya kiuhaini yaliyotokea, kosa la uhaini halipo kisheria.
Ameesema sehemu hii ya kwanza ya majumuisho yake kwa kuwakumbusha majaji watatu mzigo mzito wa kihistoria waliobebeshwa. Ameeza kuwa maamuzi watakayoyatoa katika kesi hii ya kwanza ya Kifungu cha 39(2)(d) hayatamhusu yeye pekee, bali yataweka msingi wa kisheria utakaoongoza mahakama za Tanzania na nchi kwa miaka mingi ijayo.
Ameiomba mahakama kubeba mzigo huo wa kihistoria kwa ujasiri, heshima, na bila upendeleo wowote kwa kuzingatia viapo vyao vya ujaji, ili kuweka mwongozo sahihi pindi kivumbi cha kesi hiyo kitakatapotulia.