Latest Posts

LISSU AANIKA MASUALA MASUALA TISA MAKUU YATAKAYOAMUA KESI YAKE YA UHAINI

Katika mwendelezo wa mawasilisho yake ya mwisho (final submissions) kwenye kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayosikilizwa mbele jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam., mshitakiwa Tundu Antiphas Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, ameiomba mahakama kuamua masuala tisa (9) makuu ya kisheria na kiushahidi ambayo kulingana naye, yanathibitisha kuwa kesi hiyo ya Jamhuri haina msingi wowote na inapaswa kutupiliwa mbali.

Masuala hayo ambayo Mahakama Kuu imetakiwa kuyatolea uamuzi katika hukumu yake ya mwisho ni ama mshtakiwa aliitisha mkutano wa Aprili 3, 2025 Makao Makuu ya CHADEMA Mikocheni kama inavyodaiwa na upande wa mashtaka, kama Lissu ndiye aliyealika waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuhudhuria mkutano huo, kama mshtakiwa amefanya au ametengeneza nia yoyote ya kumchochea mtu au kikundi cha watu kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali, kama maneno yanayodaiwa kutolewa na mshtakiwa yanatengeneza kosa lolote linalojulikana na sheria za Tanzania, na kama jibu ni ndiyo, je kosa hilo ni la uhaini? Kama maneno yanayodaiwa kuzungumzwa na Lissu yanatengeneza matendo (overt acts), au ikiwa kutamka maneno pekee bila matendo halisi kunaweza kuwa uhaini.

Masuala mengine ni kama mshtakiwa ndiye aliyechapisha maneno hayo kwenye akaunti ya YouTube ya Jambo TV au mitandao mingine, kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitishwa na maneno yanayodaiwa kuwa ya kihaini yaliyozungumzwa na mshtakiwa, kama upande wa mashtaka (Jamhuri) umethibitisha kesi hii katika kiwango kinachohitajika na sheria (beyond reasonable doubt) na ni hukumu au uamuzi gani sahihi ambao Mahakama inatakiwa kutoa kulingana na majibu ya masuala yote nane yaliyotangulia.

Akiingia kwenye uchambuzi wa kina wa masuala hayo, Lissu amekumbusha kuwa katika ukurasa wa 131 wa rekodi za mahakama, upande wa mashtaka ulidai kuwa mnamo Aprili 3, 2025, Lissu kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa CHADEMA aliitisha mkutano na kuzungumza na watia nia wa uchaguzi mkuu Makao Makuu ya chama Mikocheni.

Lissu amefafanua umuhimu mkubwa wa kisheria wa kubaini nani aliyeitisha mkutano huo kulingana na Kifungu cha 49 cha Kanuni ya Adhabu. Amesema kisheria, kila kitendo kinachofanywa kinahesabika kuwa ni tendo la wazi linalothibitisha nia. Ikiwa mshtakiwa aliitisha mkutano wenye lengo la kufanya uhaini, kuitisha huko kungehesabika kama kitendo cha wazi cha kisheria. Aidha, amesema kama mkutano ulikuwa wa kihaini, wote walioshiriki kuuandaa wangekuwa washirika kwenye kosa hilo la uhaini.

Aidha amezungumza kuhusu kuchepusha uhaini akifafanua kuwa kama mkutano uliitishwa kwa madhumuni ya kihaini, wote waliomsikiliza, walioshiriki, na waliorusha matangazo hayo wangekuwa wamewezesha au kunyamazia kosa la uhaini, kosa ambalo chini ya sheria lina adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

Lissu amebainisha kuwa katika mashahidi wote 17 walioletwa na upande wa mashtaka, hakuna shahidi hata mmoja aliyetoa ushahidi wa namna mkutano huo ulivyoitishwa au nani aliyewaalika waandishi wa habari. Licha ya Jamhuri kuahidi kuleta vielelezo 11 wakati wa usikilizaji wa awali (preliminary hearing), hawajaleta kielelezo hata kimoja cha kuthibitisha suala hilo iwe kwa maneno au kwa nyaraka.

Amesema tofauti na upande wa mashtaka, ushahidi pekee uliopo kwenye rekodi za mahakama unatokana na utetezi. Lissu ameuchambua ushahidi wenye kielelezo DW2 ambao ni wa John John Mnyika, Katibu Mkuu wa CHADEMA) akisema kuwa katika ukurasa wa 660 wa rekodi za mahakama, Mnyika alieleza wazi kuwa mkutano huo uliitishwa na Sekretarieti ya CHADEMA ukiwa ni wazo na maelekezo yake mwenyewe kama mtendaji mkuu, na kwamba yeye ndiye aliyewapa wasaidizi wake majukumu ya maandalizi.

Aidha, ameeleza kuwa ushahidi wa Mnyika uliungwa mkono kikamilifu na kielelezo DW3 cha ushahidi wa Naibu Katibu Mkuu Bara wa CHADEMA, Amani Golugwa na kielelezo DW4 cha ushahidi wa Mkurugenzi wa Habari wa CHADEMA, Brenda Rupia. Amesema wote hao walithibitisha kuwa Lissu na John Heche (Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara) walikuwa waalikwa tu na hawakuhusika na maandalizi au kualika waandishi.

Lissu amesisitiza kuwa tuhuma za kwamba yeye ndiye aliyeandaa na kuitisha mkutano huo ni za uongo na hazijathibitishwa kabisa na upande wa mashtaka. Ametoa wito kwa jopo la majaji kutupilia mbali mashtaka hayo kwasababu hayakukidhi viwango vya kisheria.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!