Latest Posts

MASHAHIDI WA JAMHURI KUPISHANA KAMA LISSU ALIALIKA WANAHABARI: “NI USHAHIDI USIOKUWA NA THAMANI YOYOTE”

Katika mwendelezo wa mawasilisho ya mwisho (final submissions) katika kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, Lissu ameeleza jinsi upande wa mashtaka (Jamhuri) ulivyojichanganya na kuleta mashahidi wenye kauli zinazokinzana kuhusu nani aliyealika waandishi wa habari katika mkutano wa Aprili 3, 2025.

Akiwasilisha uchambuzi wake wa kisheria mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Lissu amesisitiza kuwa mgongano huo mkubwa kati ya mashahidi wa serikali unayafanya maelezo yote ya Jamhuri juu ya suala hilo kuwa “ushahidi usiokuwa na thamani yoyote”.

Katika taarifa ya ziada iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wakati wa usikilizaji wa awali (preliminary hearing – ukurasa wa 131 wa rekodi za mahakama), Jamhuri ilidai kuwa Tundu Lissu ndiye aliyealika waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari kama Jambo TV, Clouds Media, na Mwananchi katika mkutano wa watia nia Makao Makuu ya CHADEMA Mikocheni.

Lissu amefafanua kuwa tuhuma hii haikuwa ya bahati mbaya, bali ilipangwa kimkakati ili kuthibitisha kile kinachoitwa “tendo la wazi” (overt act) la kisheria linalohitajika ili kuthibitisha kosa la uhaini. Amesema kisheria ikiwa mtuhumiwa ndiye aliyealika waandishi wa habari ili hotuba yake irushwe, kitendo hicho kingetumiwa kama thibitisho la nia ya kihaini. Zaidi ya hayo, kingewafanya waandishi wa habari waliohudhuria au kurusha matangazo hayo kuchukuliwa kama washirika walioingia kwenye kosa la kuchepusha, kuwezesha au kunyamazia uhaini (misprision of treason) linalobeba adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

Katika kuwekea wazi jinsi mashahidi 17 wa upande wa mashtaka walivyojipinga na kuchangana kizimbani, Lissu amesema kuwa Shahidi wa Kwanza wa Mashtaka, ACP George Bagyemu (PW1), alidai mahakamani kuwa “mtuhumiwa aliwaalika waandishi wa habari ili hotuba yake iweze kusikilizwa na Watanzania na wasiokuwa Watanzania kwenye Jambo TV”. Ushahidi huo uliungwa mkono na Inspekta John Kaaya (PW2) aliyesema katika ukurasa wa 161 wa rekodi za mahakama kuwa, “”wewe (Lissu) ndiye uliyewaalika sijui ulitumia njia gani lakini ni wewe”.

Hata hivyo, Lissu amesema ushahidi huo ulibomolewa na mashahidi wao wenyewe wa serikali. Mpelelezi Mkuu wa kesi hiyo, ACP Amini Mahamba (PW16), alikariri maelezo ya mashahidi P na P1 (ukurasa wa 467) akisema waandishi wa Jambo TV waliagizwa na Mkurugenzi wao John Marwa (Maro), ambaye naye alipata mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.

Kadhalika, Shahidi wa 17 wa Mashtaka (PW17- ambaye ni shahidi wa siri ‘P1’) alithibitisha wazi kizimbani kuwa: “taarifa kuhusu kikao zilitolewa na Mkurugenzi wetu John Marwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA… ninajua kwamba Afisa Mawasiliano wa CHADEMA alikuwa Brenda Rupia… haitakuwa sawa kwa mtu kusema kwamba mkutano ulipangwa na Tundu Lissu na alikuwa na alitoa/kutuma mialiko”.

Lissu amehoji, “Kuna sehemu moja ya ulimi inayosema mshtakiwa ndiye aliitisha waandishi na sehemu nyingine inasema sio yeye. Hizi ni ndimi mbili za mdomo mmoja wa mashtaka, ndimi mbili kama za nyoka. Ni ulimi upi ambao mahakama hii inaweza kuenda nao?”.

Akionesha athari za kiushahidi za mgongano huo, Lissu amerejea msimamo thabiti uliowekwa na Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Hamisi Said Adam Supra (ukurasa wa 11). Mahakama ya Rufani ilitengeneza msingi wa kisheria kuwa, pale ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wanajikunja na kutoa ndimi mbili zinazokinzana, ushahidi huo unajiondolea uaminifu.

Kutokana na hilo, Lissum amesema Mahakama haiwezi kuchukua ushahidi wa namna hiyo kwani ni “ushahidi usiokuwa na thamani yoyote” (valueless evidence).

Hivyo, Lissu amebainisha kuwa ushahidi wote wa upande wa utetezi uliotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa, na Mkurugenzi wa Habari wa CHADEMA Brenda Rupia umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mialiko ya wanahabari ilitolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Habari, Brenda Rupia na kwamba Lissu alikuwa mwalikwa tu.

Amesisitiza kuwa upande wa mashtaka haukuthubutu hata mara moja kuhoji ushahidi huo wa Brenda Rupia wakati wa maswali ya dodoso, jambo linalomaanisha kisheria kuwa upande wa mashtaka umekubaliana na ukweli huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!