Tanzania inaendelea kupanua wigo wa kimkakati katika kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka barani Ulaya, ikitumia ziara maalum ya uhamasishaji nchini Finland kuwasilisha fursa zake kubwa za kiuchumi, kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara, na kuunganisha miradi ya ndani na mitaji, teknolojia, na utaalamu wa kisasa kutoka mataifa ya Nordic na Ulaya kwa ujumla.
Akizungumza mbele ya wawekezaji jijini Helsinki, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara ya kuhamasisha mataifa ya Ulaya kuwekeza nchini Tanzania, amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Finland kuichagua Tanzania kama kitovu kikuu cha uwekezaji wao, akisisitiza kuwa nchi inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuweka sekta binafsi mbele kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi.

Dkt. Chaya amebainisha kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kujenga uchumi shindani na jumuishi unaotumia teknolojia na uvumbuzi kuongeza tija katika sekta za kilimo, viwanda, miundombinu, TEHAMA, na uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amewasilisha fursa mbalimbali za miradi mikubwa, huku akigusia kwa kina sekta ya madini ya kimkakati kama vile graphite, nickel, cobalt, na niobium.

Ametaja miradi mikubwa inayotoa fursa za mitaji na ushiriki wa kimataifa kuwa ni pamoja na Epanko Graphite, Kabanga Nickel, Southern Rukwa Helium, na Panda Hill Niobium. Aidha, ametolea mfano Eneo Maalum la Kiuchumi la Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone), ambalo lilikuwa mgodi wa dhahabu na sasa linabadilishwa kuwa kitovu cha uchakataji na uongezaji thamani wa madini.
Upande wa Finland, kupitia Katibu wa Kisiasa Pasi Rajala, umesifu uhusiano wa miaka 60 kati ya nchi hizo mbili na kuonesha utayari wa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi wa kidijiti na madini, huku taasisi za kifedha kama Finnvera na Finnfund zikitajwa kuangalia uwezekano wa kutoa mifumo ya ufadhili kwa miradi ya pamoja.

Katika hatua nyingine, Teri ameongeza kuwa TISEZA, kupitia Kituo cha Pamoja cha Huduma za Uwekezaji itaendelea kurahisisha safari ya mwekezaji kuanzia hatua ya awali hadi utekelezaji, ikihakikisha kuwa rasilimali na mazungumzo hayo yanageuka kuwa miradi thabiti itakayonufaisha pande zote mbili.
