Jamii imetakiwa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, shughuli za kiuchumi na uhifadhi wa mazingira, hatua inayolenga kuchochea maendeleo jumuishi yanayozingatia usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu (HROP), wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti shirikishi kuhusu usawa wa kijinsia katika kamati za jamii ngazi ya vijiji.

Utafiti huo uliofanyika katika Halmashauri za Mufindi, Wanging’ombe na Mbarali, uliangazia ushiriki wa wanawake katika kamati zinazohusika na huduma za jamii, maliasili na utalii, matumizi bora ya ardhi, mazingira, maafa pamoja na jumuiya za watumia maji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari na Mawasiliano wa TGNP Makao Makuu, Monica John, amesema bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha wanawake na makundi mengine wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi na shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa HROP Wilaya ya Mufindi, Patrick Umberto, amesema Halmashauri ya Mufindi itaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia, ikiwa na lengo la kufikia uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 wa wanawake na wanaume katika nafasi mbalimbali.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Christina Mpogole na Kelvin Liweuli, wamesema watatumia elimu waliyoipata kuhamasisha wananchi wenzao kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi na kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeongoza kwa kiwango cha usawa wa kijinsia katika kamati zilizofanyiwa tathmini, ikifuatiwa na Halmashauri za Wanging’ombe mkoani Njombe na Mbarali mkoani Mbeya.
TGNP imeendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kutambua mchango wa wanawake katika uongozi, uchumi na uhifadhi wa mazingira, huku ikihimiza wadau mbalimbali kuendeleza elimu na hatua zinazowezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayogusa maisha na maendeleo ya jamii.