Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, mke wake pamoja na watu wengine waliopoteza maisha katika ajali ya helikopta iliyotokea Marondera, Zimbabwe.
Katika salamu hizo alizotoa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii leo Oktoba Mosi, Dkt. Samia amesema Zimbabwe na Afrika kwa ujumla zimepoteza mjasiriamali kijana na mwenye maono, ambaye amegusa maisha ya watu wengi kupitia shughuli zake.
Dkt. Samia pia ametoa pole kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, familia ya Chivayo, familia za wote waliopoteza wapendwa wao pamoja na wananchi wa Zimbabwe, akisema Serikali na wananchi wa Tanzania wanashirikiana nao katika kipindi hiki cha majonzi.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa salamu zangu za pole za dhati na za moyoni kwa Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe; familia ya Chivayo, familia za wote waliopoteza wapendwa wao na wananchi wa Zimbabwe.”
Amehitimisha kwa kuwaombea marehemu wote wapumzike kwa amani.
Ikumbukwe siku chache baada ya Rais Samia kufiwa na mumewe Hafidh Ameir, Bwana Chivayo alienda nyumbani kwa Rais Kizimkazi, Zanzibar na kumpa pole ambapo baadae alichapisha picha zao katika ukurasa wake wa Instagram.