Latest Posts

KITASENGWA FC YATWAA UBINGWA SAO HILL MISITU SPORTS BONANZA 2026

Timu ya Kitasengwa FC imetwaa ubingwa wa soka katika mashindano ya Sao Hill Misitu Sports Bonanza 2026, awamu ya 13, baada ya kuichapa Kitilu kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia ushindani mkali katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ihefu, Wilaya ya Mufindi.

Mashindano hayo yaliyoanza Oktoba 1 na kuhitimishwa Oktoba 10, 2026, yalishirikisha timu 25 zilizoshindana katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, riadha na kuvuta kamba, yakilenga kuunganisha jamii kupitia michezo na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wa wanawake, timu ya Sao Hill Queens ilitwaa ubingwa wa netiboli baada ya kuishinda Mninga kwa vikapu 26-25, katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa hadi dakika za mwisho.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Robert Kileo, amewataka wananchi kutumia michezo kuimarisha umoja na kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi misitu inayozunguka Shamba la Miti Sao Hill.

Amesema misitu ni nguzo muhimu ya uchumi wa Mufindi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa dhidi ya uharibifu, hususan uchomaji moto holela unaoweza kusababisha hasara kubwa kwa mazingira na uchumi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Msaidizi wa Shamba la Miti Sao Hill, Kitengo cha Uendelezaji Rasilimali Misitu na Nyuki, PCO Said Singano, amesema bonanza hilo ni sehemu ya mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo kuhusu namna ya kuzuia na kupambana na moto misituni, hasa wakati wa kiangazi.

Katika utoaji wa zawadi, Kitasengwa FC ilikabidhiwa kombe, medali na Sh. 800,000 kwa kushika nafasi ya kwanza, huku Kitilu ikipata kombe, medali na Sh. 400,000 kwa nafasi ya pili. Kwa upande wa netiboli, Sao Hill Queens ilishika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Mninga na Mgololo. Pia, zawadi zilitolewa kwa wachezaji waliofanya vizuri.

Sao Hill Misitu Sports Bonanza limeendelea kuwa jukwaa la kuunganisha michezo na uhifadhi wa mazingira, likihamasisha wananchi kuepuka uchomaji moto holela na kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya moto. Kupitia ushirikiano kati ya wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), juhudi zinaendelea kuimarisha ulinzi wa misitu inayochangia ajira, uchumi na maendeleo ya Wilaya ya Mufindi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!