Mbunge wa Jimbo la Isimani, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda amesema Tanzania imepiga hatua katika kujitegemea kiuchumi, akieleza kuwa bajeti ya Serikali inayofikia Sh trilioni 62 ni miongoni mwa viashiria vya maendeleo ya uchumi na uwezo wa Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi wake.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inalenga kuimarisha uchumi wa nchi na kufikia hatua ya kujitegemea kiuchumi kwa asilimia 100, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa kuibua, kujadili na kusambaza mambo yenye manufaa kwa taifa, badala ya kutumia majukwaa hayo katika shughuli zinazoweza kudhoofisha umoja na maendeleo ya nchi.
Mtatifikolo ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ilolompya wakati wa ziara yake jimboni, ambapo pia amewaomba wananchi kuwaombea viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili waendelee kutekeleza majukumu yao na kuleta maendeleo kwa wananchi.
