Kampuni ya Kitanzania ya Amsons Group imefanya ununuzi mkubwa katika sekta ya nishati baada ya kuingia makubaliano rasmi ya kuinunua na kuchukua miundombinu yote ya kuchakata, kuzalisha, na kusambaza mafuta ghafi na gesi asilia ya Oryx Energies nchini Tanzania.
Ununuzi huo wa kimkakati unahamishia vituo muhimu vya kujaza mafuta (petrol stations), bohari za kuhifadhia mafuta, pamoja na mtandao mpana wa usambazaji na uzalishaji mikononi mwa kampuni hiyo. Hatua hii inadhihirisha ukuaji wa kampuni za wazawa katika kumiliki na kuendesha miundombinu mikuu ya uchumi na nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Amsons Group, ambayo ina uwepo thabiti na uwekezaji katika sekta mbalimbali, imeelezwa kuwa katika nafasi nzuri ya kuendeleza misingi iliyowekwa na Oryx Energies na kufungua fursa mpya za kibiashara nchini. Ununuzi huo ni sehemu ya tathmini ya kimkakati inayofanywa na Oryx Energies juu ya rasilimali zake za usambazaji mafuta barani Afrika.
Akizungumzia uamuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Energies, Bw. Moussa Diao, amesema kuwa wanafurahi kufikia makubaliano hayo na Amsons Group kutokana na kampuni hiyo kuwa na misingi imara nchini Tanzania na nia ya kukua.

“Tunaamini kuwa Amsons Group ipo katika nafasi nzuri ya kuivusha biashara hii kwenda hatua inayofuata, ikijenga juu ya uwezo uliopo na kutengeneza fursa mpya kwa wafanyakazi, wateja, na washirika wake. Mkataba huu pia ni hatua muhimu katika muundo wa mkakati wa Oryx Energies, tukilenga kuelekeza mitaji na juhudi zetu katika kuendeleza miundombinu ya nishati kote barani Afrika na kuimarisha shughuli zetu za kibiashara. Afrika inabaki kuwa moyo wa biashara yetu na malengo yetu ya muda mrefu”, ameeleza Diao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Bw. Edha Nahdi, ameeleza kuwa ununuzi huo ni hatua kubwa katika azma yao ya kupanua biashara za nishati na usafirishaji.

“Kuunganishwa kwa mtandao mpana wa usambazaji wa Oryx na uwezo wake wa bohari za kuhifadhia mafuta kunatuwezesha kuimarisha usalama wa nishati nchini na kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu na cha kimkakati cha vifaa na usafirishaji kwa Afrika Mashariki na Kati”, ameeleza.
Kukamilika kikamilifu kwa uuzaji huu kunasubiri idhini kutoka kwa mamlaka za udhibiti za serikali. Wakati mchakato huo ukiendelea, huduma za Oryx Energies zitaendelea kutolewa kama kawaida bila usumbufu kwa wateja, wafanyakazi, na washirika wao.