Latest Posts

MFANYAKAZI WA NDANI AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUUA MTOTO WA MIAKA MITANO

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mfanyakazi wa ndani, Verediana Levee, kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mtoto William Mathayo, mwenye umri wa miaka mitano, aliyekutwa amefariki ndani ya nyumba yao katika Mtaa wa Ibolelo, Kata ya Nyankumbu, Wilaya ya Geita.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Oktoba 24, 2026, majira ya saa 4:00 asubuhi, wakati mtoto huyo akiwa amelala kitandani nyumbani kwao. Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa anadaiwa kumuua mtoto huyo kwa kumkaba shingo, wakati wazazi wake wakiwa hawapo nyumbani kutokana na shughuli zao mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, imeeleza kuwa chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni imani za kishirikina. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeripoti matukio mengine matatu ya vifo yaliyotokea kati ya Oktoba 17 na 26, mwaka huu, ambayo yanahusishwa na changamoto mbalimbali za kimaisha.

Tukio la kwanza lilitokea Oktoba 17, 2026, katika eneo la Makurugusi, Wilaya ya Chato, ambapo Isack Ibrahimu, mwenye umri wa miaka 36, alikutwa amefariki baada ya kujijeruhi shingoni na tumboni kwa kutumia kitu chenye ncha kali. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo linahusishwa na msongo wa mawazo uliotokana na ugumu wa maisha.

Tukio la pili liliripotiwa Oktoba 21, 2026, katika Mtaa wa Moringe, Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita, ambapo Timotheo Chande, mwenye umri wa miaka 21 na dereva wa bajaji, alikutwa amefariki nyumbani kwao baada ya kujinyonga. Chanzo cha tukio hilo kimeelezwa kuwa ni msongo wa mawazo uliotokana na maradhi.

Aidha, Oktoba 26, 2026, Japhet Ladislaus, mwenye umri wa miaka 19, mkazi wa Mtaa wa Mbabani, Kata ya Mtakuja, alikutwa amefariki baada ya kujinyonga nje ya nyumba yao. Taarifa ya polisi imehusisha tukio hilo na msongo wa mawazo uliotokana na changamoto za mahusiano.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa miili ya marehemu hao ilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewataka wazazi na walezi kuwa makini wanapowakabidhi watoto wao kwa watu wengine kwa ajili ya malezi, ili kuimarisha usalama wa watoto na kuzuia vitendo vya ukatili.

Vilevile, wananchi, hususan vijana, wametakiwa kutafuta msaada na njia salama za kukabiliana na changamoto za maisha, maradhi na mahusiano, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuhatarisha maisha yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!