Latest Posts

THRDC YATOA WITO MZITO KENYA: YATAKA UCHUNGUZI WA HARAKA KUBAINI ALIPO TWAHA MWAIPAYA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa wito kwa mamlaka nchini Kenya kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini mahali alipo mwanaharakati na raia wa Tanzania, Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, Oktoba 26, 2026, tukio hilo lilitokea Jumapili, Oktoba 25, 2026, jijini Nairobi, Kenya. THRDC imesema watu wasiojulikana walikuwa wakimfuatilia Mwaipaya, kisha kuvamia gari alilokuwa nalo na kuondoka naye kusikojulikana.

Kutokana na mazingira hayo, THRDC imeeleza kushtushwa na kile imesema ni ukimya pamoja na ukosefu wa taarifa rasmi kutoka kwa vyombo vya usalama nchini Kenya hadi kufikia Jumatatu, Oktoba 26, 2026, ikiwa ni siku mbili tangu kuripotiwa kwa tukio hilo.

THRDC imeeleza kuwa, licha ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya kufuatilia suala hilo, kutoonekana kwa taarifa rasmi za kiserikali kumezidi kuleta hofu kwa familia yake, jamii, na wanaharakati.

Zaidi THRDC imeeleza kwamba, Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, Ibara za 21, 26, 29, 49 na 51 zinaweka wazi wajibu wa kulinda haki ya kuishi, uhuru, usalama, na haki za mtu anayeshikiliwa, ikiwemo kuonana na wakili na kufikishwa mahakamani.

Aidha imesema kupitia Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 na mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia wa 1961 na Mahusiano ya Kibalozi wa 1963, Tanzania ina wajibu wa kulinda maslahi na raia wake walioko nje ya nchi.

Katika taarifa hiyo, THRDC imetoa maazimio na ushauri, ikiiomba Serikali ya Kenya kufanya uchunguzi huru na wa wazi ili kubaini alipo Mwaipaya na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliohusika.

Aidha imeisihi Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania kupitia ubalozi wake jijini Nairobi kuongeza juhudi za kufuatilia suala hilo na kutoa taarifa sahihi kwa umma.

THRDC imesema zaidi kwamba, Iwapo Mwaipaya anashikiliwa na vyombo vya dola, sheria na taratibu zifuatwe ikiwemo kupata huduma za kisheria, matibabu, na haki ya kuwasiliana na ndugu zake na ubalozi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!