Latest Posts

MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA HANDENI AANGUKA NA KUFARIKI DUNIA KWENYE KIKAO CHA CCM TANGA

Kifo cha ghafla cha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mussa Mwanyumbu, kimeacha simanzi na pengo kubwa katika halmashauri hiyo, huku viongozi, watumishi, na wananchi wakimkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia na kuchochea shughuli za maendeleo.

Mwanyumbu, ambaye pia alikuwa Diwani wa Kata ya Mkata, alianguka kwa ghafla jioni ya jana, Jumapili, Novemba 1, 2026, akiwa katika ofisi za CCM Mkoa wa Tanga alipokuwa akihudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho. Kikao hicho kilikuwa kimehusisha pia utambulisho rasmi wa Mlezi mpya wa CCM mkoani humo, Rabia Abdallah.

Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Saitoti Steven, alieleza kuwa msiba huo ni pigo kubwa kwa halmashauri hiyo kwani marehemu alikuwa kiongozi mchapakazi asiye na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakifahamika.

“Kwa halmashauri yetu, msiba huu ni mkubwa sana. Mwenyekiti wetu hakuwa na changamoto yoyote ya kiafya na alikuwa akitekeleza majukumu yake bila shida. Kusikia kwamba ameanguka ghafla na baadaye kufariki dunia kumetushtua sana,” alisema Steven.

Kwa upande wake, Katibu wa Uenezi, Siasa na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Tanga, Samweli Mngazija, alibainisha kuwa marehemu alishiriki kikao hicho chote bila kuonyesha dalili zozote za kuumwa, lakini alianguka ghafla mara tu baada ya shughuli za kikao hicho kumalizika. Alimsifu kuwa mwanachama mwaminifu, mtiifu, na mwenye kutoa mawazo yenye tija yaliyosaidia kukijenga chama.

Naye Shaban Alfan, mmoja wa wakazi na wananchi wa kata aliyokuwa akiiwakilisha kama diwani, alieleza kuwa jamii itaendelea kumkumbuka kwa utumishi wake uliotukuka katika kusimamia maendeleo na kutetea maslahi ya wananchi wa eneo hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!