Wakili anayemtetea Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni ya Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Pambalu, Hekima Mwasipu amekanusha madai yaliyotolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA kupitia Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Hilda Newton kwamba kurejea kwa mteja wake nchini na kutoa maelezo kwa Jeshi la Polisi kunahusiana na madai ya kutekwa kwa mwanaharakati na mwanachama wa chama hicho, Twaha Mwaipaya, jijini Nairobi nchini Kenya.
Sintofahamu hiyo imeibuka katikati ya madai ya kutekwa kwa Twaha Mwaipaya nchini Kenya na kushikiliwa kwa Pambalu nchini Tanzania kufuatia kufunguliwa kwa mashtaka ya uhaini yanayohusiana na matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mnamo Novemba 1, 2026, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Hilda Newton alichapisha maelezo akimshutumu Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, kwa kumshawishi Pambalu kurejea nchini Tanzania na kutoa ushirikiano kamili kwa Jeshi la Polisi. Katika chapisho hilo, Hilda alidai kuwa Lema alimhakikishia Pambalu usalama wake akisema alizungumza na afisa wa polisi na kwamba kila kitu kilikuwa sawa, jambo lililompa Pambalu ujasiri wa kurejea nchini.
“Pambalu kwa maelekezo yake wakati anazungumza na watu walioenda kumuona gerezani hivi karibuni anasema, wakati polisi wanamhoji alizungumza ukweli wake wote ambao anaujua kuhusu watu waliopo Nairobi. Siku kadhaa baada ya Pambalu kusema ukweli wake wote, Twaha Mwaipaya akatekwa na watu wasiojulikana mpaka leo imetimia siku nane hatujui Twaha yupo wapi”, aliandika Hilda katika sehemu ya chapisho lake.
Kufuatia chapisho la Hilda, Wakili Mwasipu alijibu kupitia mitandao yake ya kijamii ili kuweka wazi masuala yote ambayo mteja wake alihojiwa mbele yake wakati akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Wakili Mwasipu alitaja mambo ambayo Pambalu alihojiwa mbele yake ikiwamo majukumu aliyopangiwa na Kamati Kuu ya CHADEMA katika Hoteli za Desderia na Bagamoyo, kama alihusika kuandaa filamu ya kumbukumbu ya mauaji ya tarehe 29 Oktoba 2025 kabla akiwa na John Kitoka, uhusika wake na Dkt. Slaa na Mchungaji Mwamakula kwenda nchini Uganda na Kenya kuhamasisha maandamano, kama yeye ni ‘Admin Msaidizi wa akaunti ya mtandao wa kijamii ya ‘Chadema in Blood’ akiwa na Twaha Mwaipaya na kazi za Idara ya Mafunzo ya CHADEMA.
Baada ya chapisho hilo la Wakili Mwasipu, Jambo TV leo Novemba 2, 2026 imemtafuta wakili huyo kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi wa kina wa alichokiandika. Katika ufafanuzi wake, Wakili Mwasipu ameeleza kuwa Jeshi la Polisi halikumhoji Pambalu kuhusu mahali alipo Twaha Mwaipaya wala jinsi ya kumpata.
“Walimuuliza kama yeye ndio ni admin (mwendeshaji) msaidizi wa ukurasa unaoitwa Chadema in blood ambao polisi walikuwa wanajua kwamba inaendeshwa na Mwaipaya… lakini swali lao ni kwamba je, huyu Pambalu ni msaidizi wa huo ukurasa? Akakataa…hawakuhoji kabisa kwamba Mwaipaya anapatikana wapi”, ameeleza Wakili Mwasipu.
Ikumbukwe kuwa Pambalu anakabiliwa na shtaka la uhaini lililoainishwa chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyorekebishwa mwaka 2023. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa kati ya Septemba 1, 2025 na Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam, Pambalu alidhamiria kuwashawishi wananchi kukwamisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Hati hiyo inaeleza kuwa alionesha nia hiyo kwa kuendesha na kuratibu maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima kwa lengo la kuitisha na kuishinikiza Serikali.
Aidha, madai ya Hilda Newton yamekuja wakati ambapo Godbless Lema akituhumiwa na baadhi ya wafuasi wa CHADEMA na wanaharakati mtandaoni kuwa ni msaliti au ‘dalali’ ndani ya CHADEMA. Lema ameyakataa madai hayo akieleza kuwa amekuwa akifanya jitihada za kisera na kidiplomasia kusafisha jina la CHADEMA baada ya kile alichodai kuwa ni kushutumiwa kimakosa kupanga mapinduzi au machafuko, pamoja na kulinda vijana wa chama hicho dhidi ya ukamataji na vifo.
“Kuna propaganda inajengwa kwamba kufanya ‘strategic engagement’ ni usaliti. Sisi tuko ‘ground’ vijana kila siku wanakamatwa, wanaumizwa, wanakufa… Lazima tuchoke kuzika na twende mbele kwa ajili ya lengo la kuibadilisha nchi”, alieleza Lema wakati wa mkutano wake na wanahabari mkoani Arusha mwishoni mwa juma.