Latest Posts

RC MARA AZINDUA MUSOMA MARATHON, ASISITIZA KUCHANGISHWE FEDHA ZITAKAZOSAIDIA KUPAUA VYUMBA VYA MADARASA

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, amezindua rasmi mbio za Musoma Marathon 2026, zinazotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 18 hadi 20 mwaka huu, zikiwa zimebeba michezo mbalimbali ikiwemo mbio za kilometa 21, 10, na 5, pamoja na mashindano ya baiskeli, kuogelea, mitumbwi (kasia), na mbio za watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo, Novemba 2, 2026, Mwenyekiti wa Musoma Marathon, Suzana Senso, ameeleza kuwa lengo kuu la kuandaa mbio hizo ni kuchangisha fedha zitakazosaidia kupaua vyumba vya madarasa katika shule za sekondari mkoani humo, ili kujiweka tayari kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwakani 2027 na kuelekea mwaka 2028.

Aidha, Senso alitangaza zawadi nono kwa washindi wa mbio za kilometa 21, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha shilingi milioni 1.5, wa pili milioni 1.2, wa tatu milioni 1, wa nne laki 7, na wa tano laki 5, huku washindi wengine hadi wa kumi nao wakitarajiwa kuzawadiwa. Mashindano hayo yataambatana na matukio ya burudani ikiwemo uchomaji wa nyama na samaki.

Akizindua mbio hizo, Brigedia Jenerali Mtambi amewakaribisha wanamichezo na wananchi kutoka nje ya Mkoa wa Mara kushiriki kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria, akisisitiza kuwa linagusa moja kwa moja maendeleo ya elimu na ukamilishaji wa miundombinu ya shule.

Pia, Mtambi aliwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuendelea kujenga maboma ya miundombinu ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wa mwaka 2028, wakati uongozi wa mkoa ukiendelea na jitihada za kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi huo. Musoma Marathon 2026 inatajwa kuwa ni nguzo muhimu ya mikakati ya mkoa katika kutatua changamoto za miundombinu ya elimu kupitia nguvu za pamoja za michezo na jamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!