Latest Posts

WATAALAMU TIBA ASILI WAONYWA KUEPUKA MAMBO YANAYOWEZA KUHATARISHA MAISHA YA WAGONJWA

Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini wametakiwa kuwa waangalifu na kujiepusha na vitendo au kauli zinazoweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanapotoa huduma zao kwa jamii.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 2, 2026, na Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (TAMESOT) ambaye pia ni Mratibu wa Hamasa ya Mafunzo ya Sayansi Shirikishi Kitaifa, Bw. Lukasi Joseph Mlipu, alipokuwa akizungumza akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya hamasa katika mkoa huo.

Misingi ya Utendaji na Tahadhari kwa Wataalamu

Bw. Mlipu alieleza kuwa katika ziara yake, amewahimiza wataalamu hao kuzingatia maadili na usalama wa wagonjwa, ikiwa ni pamoja na kuepuka kutoa ahadi za uongo za kuponya magonjwa yote, kutoa madai ya tiba yasiyothibitishwa kisayansi, na kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya wateja wao.

“Ili kufanikiwa, ni pamoja na kuzingatia suala la kuheshimu usalama wa mgonjwa, kujenga utamaduni wa kutoa huduma kwa uadilifu, kuelewa mipaka ya maarifa yao na kuwaelekeza wagonjwa kupata huduma za hospitali pale inapohitajika,” alisisitiza Bw. Mlipu.

Aidha, alibainisha kuwa TAMESOT imeendelea kuwahimiza wataalamu hao kushirikiana kwa karibu na Serikali na wadau wa sekta ya afya, akisisitiza kuwa sekta ya tiba asili inapaswa kuendelezwa kupitia mawasiliano mazuri, tafiti za kisayansi, na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa nchini.

Wito wa Kushiriki Mafunzo na Kauli Mbiu

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha wataalamu kujisajili na kushiriki katika mafunzo maalum ya sayansi shirikishi yatakayofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba 2026, Musoma, akibainisha kuwa kila mtaalamu ana nafasi ya kuchangia mafanikio ya programu hiyo kwa kueneza taarifa sahihi.

Akihitimisha nasaha zake, Bw. Mlipu alitoa kauli mbiu inayosisitiza misingi ya taaluma hiyo:“Tukumbuke tiba asili si uchawi, tiba asili si utapeli, maarifa ya jadi yanahitaji elimu, utafiti, uadilifu na matumizi salama. Tukiungana, tukijifunza na kushirikiana, tunaweza kuchangia katika kuhifadhi maarifa yetu ya jadi na kuendeleza matumizi yenye uwajibikaji ya dawa za asili kwa manufaa ya jamii.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!