Latest Posts

DC LUGANGIRA ASIMAMIA UREJESHAJI WA MIFUGO 52 ILIYOIBIWA, AMANI YAREJEA KATI YA JAMII MBILI ZA WAMAASAI

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, amesimamia urejeshaji wa mifugo yote 52 iliyochukuliwa katika tukio la uvunjifu wa amani lililohusisha jamii mbili za Wamaasai katika maeneo ya Kata za Kimnyaki na Lengijave, hatua iliyosaidia kurejesha hali ya amani na utulivu katika jamii hizo.

Mifugo iliyorejeshwa inajumuisha ng’ombe 26, mbuzi 20 na kondoo sita, kufuatia juhudi za Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa kimila wa jamii ya Wamaasai, alimaarufu kama Malaigwanani, katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Katika kusimamia utatuzi wa tukio hilo, Mhe Lugangira alifika katika Kituo cha Polisi Ngaramtoni kupata taarifa za awali kuhusu tukio hilo pamoja na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.

Baada ya kupata taarifa hizo, Mkuu huyo wa Wilaya alizungumza na wanajamii wa Kimnyaki na kuwahakikishia kuwa Serikali imechukua hatua kulishughulikia suala hilo, huku akiwataka kuendelea kuwa watulivu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuongeza taharuki na kuvuruga amani.

Aidha, alieleza dhamira ya Serikali kukutana na jamii nyingine ya Wamaasai katika eneo la Lengijave ili kusikiliza pande zote mbili na kutatua mgogoro huo kwa njia ya maelewano na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Lugangira amesisitiza kuwa tofauti zinazoweza kujitokeza baina ya jamii hazipaswi kuwa chanzo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, bali zinapaswa kutatuliwa kwa njia za mazungumzo, maelewano na kufuata taratibu zinazotambulika kisheria.

Amesema Serikali inatambua na kuheshimu mila lakini amesisitiza kuwa matukio yenye viashiria vya uhalifu au kwenda kinyume na sheria yanapaswa kuripotiwa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe badala ya kutegemea taratibu za kimila pekee.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wa kimila wa jamii ya Wamaasai (Malaigwanani) kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuzuia migogoro, kuimarisha maelewano na kuhakikisha amani na mshikamano vinaendelea kudumishwa katika jamii hizo.

Urejeshaji wa mifugo hiyo 52 ni hatua muhimu katika kurejesha mahusiano mema kati ya jamii hizo mbili na mkoa wa Arusha hali ni shwari na salama.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!