Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kufanya matengenezo kinga katika bomba kuu la maji linalosafirisha maji kutoka Mtambo wa Uzalishaji Maji wa Ruvu Chini, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo wakati wa mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kutokana na El Niño.
Chalamila amesema hayo leo baada ya kutembelea na kukagua kazi za matengenezo katika bomba hilo lenye kipenyo cha inchi 72, lililopo eneo la Mpiji, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Amesema huduma ya maji ni muhimu kwa maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi jijini Dar es Salaam, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za mapema kuimarisha miundombinu ili iweze kuhimili changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Amesema DAWASA imechukua hatua sahihi kwa kufanya matengenezo hayo kabla ya mvua kubwa kuanza, kwani uharibifu wa bomba hilo au miundombinu inayolizunguka wakati wa mvua ungeweza kuathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji kwa wananchi.

“Niwapongeze DAWASA kwa kuchukua tahadhari za mapema. Inawezekana wakati wa mvua kubwa ukarabati huu usingewezekana kufanyika na hali hiyo ingeathiri upatikanaji wa huduma ya maji. Nitoe rai kwa wananchi wanaohudumiwa na bomba hili kuanzia ukanda wa Bagamoyo hadi Ilala kuwa wavumilivu kutokana na kupungua kwa kiwango cha upatikanaji wa maji,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amemshukuru Chalamila kwa kutembelea na kukagua maendeleo ya matengenezo hayo, akisema ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha miundombinu na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa.
Amesema kazi ya matengenezo itaanza Jumanne, Novemba 3,2026 na inatarajiwa kukamilika ndani ya saa 96 ambayo ni Novemba 6,2026 ambapo huduma ya maji inatarajiwa kurejea katika hali yake ya kawaida ifikapo Ijumaa jioni.
Ameeleza kuwa matengenezo hayo ni muhimu katika kuhakikisha bomba kuu linaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa na uwezo wa kuhimili changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.
DAWASA imewaomba wananchi wanaotegemea maji kutoka bomba hilo, hususan katika maeneo ya Bagamoyo hadi Ilala, kuwa wavumilivu wakati wa matengenezo hayo, huku Mamlaka ikiendelea kusimamia kazi hizo ili zikamilike kwa wakati na huduma irejee kama ilivyopangwa