Imeelezwa kuwa Dunia iko katika njia ya kuelekea kuwa na mwaka wenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa, huku wanasayansi wakihusisha hali hiyo na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za hali ya hewa ya El Niño.
Taasisi huru ya utafiti ya Marekani, Berkeley Earth imeeleza leo Novemba 9, 2026 kuwa ina uhakika kwa asilimia 95 kwamba mwaka 2026 utapita rekodi ya joto iliyowekwa mwaka 2024. Onyo hili linatolewa wakati viongozi wa dunia na wapatanishi wakikusanyika mjini Antalya, Uturuki, kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi (COP31).
Hata hivyo athari hizo zinazotajwa zimeshaanza kujidhihirisha kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni sehemu mbalimbali za dunia. Nchi nyingi zimejikuta zikikabiliana na majanga makubwa ya asili, ikiwemo mioto mikubwa ya nyikani iliyoteketeza maeneo ya Ulaya Magharibi hadi Indonesia, pamoja na kuanguka ghafla kwa barafu nchini Nepal kulikosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000. Aidha, huduma ya hali ya hewa ya Umoja wa Ulaya (Copernicus) imethibitisha kuwa mwezi Oktoba 2026 ndio uliokuwa mwezi wenye joto kali zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu rekodi zianze kuwekwa.

Kwa upande wake, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limetoa ripoti yake likitabiri kuwa mwaka 2026 utakuwa miongoni mwa miaka minne yenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa. Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, ameonya kuwa hakutakuwa na nafuu mwaka 2027 kwasababu hali ya El Niño yenye nguvu isiyo ya kawaida itaendelea kutoa joto lililofyonzwa baharini na kusukuma halijoto ya dunia juu zaidi.
Kichocheo kikuu cha kupanda huku kwa halijoto ni kuongezeka kwa mkusanyiko wa gesi ya kabonidioksidi angani kunakotokana na uchomaji wa mafuta ya visukuku (vyanzo vya nishati vinavyotokana na mabaki ya mimea, wanyama, bakteria, na viumbe vya baharini).
Wanasayansi wanaonya kuwa dunia kwa sasa inaelekea kufikia ongezeko la nyuzi joto 2.8 ifikapo mwisho wa karne hii, kiwango ambacho kinavuka kwa mbali lengo la nyuzi joto 1.5 lililowekwa chini ya Mkataba wa Paris. Hali hii tayari imesababisha viongozi, akiwemo waziri mmoja nchini Uingereza, kuwataka wananchi na wafanyabiashara kujiandaa kwa dharura za hali ya hewa na usumbufu wa upatikanaji wa chakula.
Katika mkutano huo wa wiki mbili wa COP31, mkuu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, amezihimiza serikali kuchukua hatua za haraka kwani joto kali tayari linaigharimu dunia kiuchumi na kijamii. Ingawa mikutano iliyopita ilijikita zaidi katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, mataifa mengi sasa yanalazimika kutafuta mbinu za kuzoea mabadiliko haya ya hali ya hewa ambayo hayaepukiki.
Msimamo huo wa Umoja wa Ulaya unatajwa kupingana na mataifa yanayozalisha mafuta na gesi kama Saudi Arabia na Urusi, ambayo yanapigania matumizi ya gesi kama nishati mbadala ya muda mfupi badala ya makaa ya mawe. Huku mivutano hiyo ikiendelea, Katibu Mkuu wa WMO amesisitiza kuwa ukosefu wa makubaliano ya haraka baina ya mataifa ndio unaozidisha ukubwa wa majanga ya hali ya hewa yanayoikumba dunia hivi sasa.