Latest Posts

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WAMI/RUVU KWA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA UFUATILIAJI WA RASILIMALI ZA MAJI

 

 

Katika kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji nchini, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeendelea na ziara ya kutembelea na kukagua vituo vya ufuatiliaji wa mwenendo wa maji katika mito vinavyosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Kamati wametembelea kituo cha kupima hali ya wingi wa maji katika Mto Ruvu, kilichopo eneo la Ruvu Kibungo, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambapo wamepata maelezo kuhusu namna kituo hicho kinavyofanya kazi katika kukusanya na kutoa takwimu za mwenendo wa maji mtoni.

Vituo hivyo vina umuhimu mkubwa katika usimamizi wa rasilimali za maji kwani huwezesha Bodi kupata takwimu sahihi na za uhakika kuhusu kiasi cha maji kinachopita katika mito kwa nyakati tofauti. Taarifa hizo hutumika katika kupanga na kusimamia matumizi ya maji, kufanya maamuzi sahihi kuhusu ugawaji wa rasilimali hiyo, kutambua mabadiliko ya mwenendo wa maji pamoja na kutoa tahadhari mapema dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha mafuriko au upungufu wa maji.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Patrick Mwalunenge (Mb), ameipongeza Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa juhudi zinazofanyika katika kusimamia na kuhifadhi mazingira, akieleza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa Kamati hiyo kukagua utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za usimamizi, uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za maji zinazotekelezwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!