Latest Posts

TANZANIA YAITAKA UINGEREZA KUHESHIMU UHURU WA MAHAKAMA ZA TANZANIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeitaka Serikali ya Uingereza na washirika wa kimataifa kuheshimu uhuru wa Mahakama na michakato ya kisheria ya Tanzania, ikisisitiza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ilifuata misingi ya Katiba, sheria na haki zote za kisheria.

Msimamo huo umetolewa leo, Novemba 12, 2026, kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Taarifa hiyo imekuja kufuatia tamko lililotolewa Novemba 10, 2026 na Waziri wa Afrika na Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Kirsty McNeill, aliyeeleza kuwa Serikali ya Uingereza ina wasiwasi mkubwa kuhusu kutiwa hatiani kwa Lissu katika kesi ya uchochezi.

Katika tamko hilo, McNeill alikumbusha maoni ya Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Uzuiaji Holela wa Uhuru (UN Working Group on Arbitrary Detention, namba 74/2025), kilichobaini kuwa Lissu alishikiliwa kiholela bila msingi wa kutosha wa kisheria na kwamba kulikuwa na dosari kubwa katika mwenendo wa haki wa kesi hiyo.

Serikali ya Uingereza iliongeza kuwa hatua hiyo inakiuka Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa ambapo Tanzania ni mwanachama, huku ikiikumbusha Tanzania wajibu wake wa kulinda haki za binadamu, ikiwamo kupata haki katika mwenendo wa kesi, uhuru wa kujieleza, kushiriki katika shughuli za kisiasa, kutendewa kwa usawa mbele ya sheria na kuendeleza maridhiano ya kisiasa.

Ikijibu wasiwasi huo wa Uingereza, Wizara ya Mambo ya Nje imebainisha kuwa hukumu ya Lissu ilitolewa na mahakama yenye mamlaka kamili kisheria baada ya kukamilika kwa mchakato unaostahili wa kisheria uliompa Lissu fursa zote za haki.

Wizara imebainisha kuwa ilielezwa kuwa Lissu alipata haki zote za msingi kabla na wakati wa shauri hilo, ikiwa ni pamoja na kuwakilishwa na mawakili wa kisheria, kupewa fursa ya kusikilizwa kwa haki, pamoja na kupewa ufafanuzi kamili wa haki yake ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa uhuru wa vyombo vya utoaji haki ni nguzo kuu isiyotikisika ya mfumo wa katiba wa nchi hiyo, na kwa msingi huo ikawataka washirika wote wa kimataifa kuheshimu uhuru wa Mahakama na michakato ya kisheria ya Tanzania badala ya kuingilia maamuzi yake.

“Wizara inapenda kufafanua zaidi kuwa, uhuru wa mahakama ni nguzo kuu ya mfumo wa katiba wa Tanzania, na kwa hiyo Serikali inatoa wito kwa washirika wote kuheshimu uhuru wa mahakama na michakato ya kisheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasalia thabiti katika ahadi yake ya kutetea haki za binadamu na utawala wa sheria,” imesistitiza taarifa hiyo.

Aidha, Tanzania imekumbusha kuwa inafurahia uhusiano wa kihistoria, wa karibu na wa kirafiki na Uingereza uliodumu kwa miongo mingi, ukizingatia misingi ya kuheshimiana, maadili ya pamoja, ushirikiano wa maendeleo, biashara, uwekezaji, elimu na uhusiano wa wananchi wa pande zote mbili. Hata hivyo, imeweka wazi kuwa masuala yote yanayohusu masilahi ya pande mbili yanapaswa kujadiliwa kupitia mashauriano ya kidiplomasia yanayoheshimu mipaka ya kila nchi na kutokuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!