Latest Posts

TUME YA HAKI ZA BINADAMU: HATUJAPINGA WALA KUUNGA MKONO HUKUMU YA LISSU

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imezitaka taasisi zote za umma, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na wananchi wa Tanzania kwa jumla kuhakikisha kuwa tofauti zote za maoni kuhusu maamuzi ya mahakama na masuala ya maslahi ya umma zinashughulikiwa kwa amani na kupitia njia za kisheria, kikatiba na kidemokrasia.

Wito huo umetolewa kupitia tamko rasmi la msimamo wa Tume hiyo lililotolewa Novemba 13, 2026, na Mwenyekiti wa THBUB, Dunford George Mpelumbe. Tamko hilo limetolewa kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania mnamo Novemba 6, 2026 katika shauri la Jinai Namba 000019605 la Mwaka 2025, ambapo Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu aliondolewa hatiani kwenye kosa la uhaini lakini akatiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani kwa kosa la uchochezi chini ya Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu na Kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

“THBUB inatoa wito kwa wadau wote, ikiwa ni pamoja na taasisi za umma, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, mashirika ya kimataifa, vyombo vya kitaaluma, taasisi za dini, vyombo vya habari na wananchi kwa jumla, kukuza mazungumzo ya ujenzi, kuheshimiana na kushirikiana kwa amani. Tofauti za maoni kuhusu maamuzi ya mahakama na masuala ya maslahi ya umma zinapaswa kushughulikiwa kupitia njia za kisheria, kikatiba na za kidemokrasia,” amesisitiza Mpelumbe

THBUB imebainisha kuwa imefuatilia kwa karibu maoni na hisia zilizotolewa na wadau mbalimbali wa ndani, kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na Serikali ya Tanzania, CCM, CHADEMA, ACT Wazalendo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Amnesty International, Human Rights Watch, FIDH, LHRC, Kikundi Kazi cha UN (UNWGAD), na Idara ya Mambo ya Nje ya Uingereza (FCDO).

THBUB imesisitiza kuwa jukumu lake la usimamizi wa haki za binadamu liko tofauti na mamlaka ya kimahakama, na kwamba Tume haina mamlaka ya kirufaa au uwezo wa kupitia, kubadilisha au kufuta maamuzi yaliyofanywa na mahakama yenye mamlaka.

Ikieleza mipaka yake ya kisheria, Tume imekumbusha kuwa Ibara ya 130(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaizuia THBUB kuchunguza maamuzi ya majaji, makadhi au mahakama yaliyofanywa katika kutekeleza majukumu ya kimahakama. Pia, Ibara ya 131(2)(a) ya Katiba na Kifungu cha 17(2)(a) cha Sheria ya THBUB kinaizuia Tume kuchunguza masuala yaliyo mbele ya mahakama au yanayosubiri rufaa.

Kutokana na misingi hiyo ya kikatiba, THBUB imeweka wazi kuwa haijaunga mkono wala kupinga hukumu iliyotolewa dhidi ya Lissu, ikieleza kuwa maamuzi ya kisheria yanapaswa kushughulikiwa kupitia mchakato wa rufaa mahakamani.

“Uhuru wa Mahakama, kutopendelea na heshima kwa mamlaka ya mahakama ni misingi mikuu ya utawala wa sheria na ni muhimu katika utoaji haki unaostahili… Kwa msingi huo, THBUB haijaunga mkono wala kupinga kutiwa hatiani au adhabu iliyowekwa dhidi ya Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu,” inasomeka sehemu ya tamko hilo.

THBUB imerejea uchunguzi wa kujitegemea iliofanya mnamo Juni 27, 2025 gerezani kukagua hali na usalama wa Lissu akiwa mahabusu. Katika uchunguzi huo, THBUB ilibaini kuwa haki zake za msingi ziliendelea kuheshimiwa kulingana na Katiba na sharia.

Ikieleza matokeo ya uchunguzi huo wa gerezani, CHRAGG imebainisha kuwa Lissu alikuwa akipata na kufurahia uhuru wa kuabudu chini ya Ibara ya 19 ya Katiba, haki ya faragha chini ya Ibara ya 16, haki ya kuwasiliana na mawakili au ndugu zake chini ya Ibara ya 13(6)(a) na (b), pamoja na fursa ya kufanya mazoezi ya viungo kulingana na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba na viwango vya kimataifa vya Nelson Mandela Rules.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!