Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amezindua Kamati ya Utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ya Halmashauri za Wilaya ya Arusha (Arusha DC) na Meru (Meru DC), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa uhakika na kwa gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lugangira ameitaka Kamati hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kuhakikisha mpango huo unawafikia wananchi wote wanaostahili kupata huduma kupitia mfumo wa bima ya afya.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kutambua umuhimu wake na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa ushirikiano baina ya viongozi, watendaji wa Serikali na wataalamu wa sekta ya afya ni muhimu katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio katika Halmashauri zote mbili.

Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Wilaya ya Arumeru.