Serikali ya Norway imeonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vitongojini (Hamlet Electrification Project) pamoja na mradi wa Nishati safi ya kupikia mkoani Lindi unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambao umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.
Pongezi hizo zimetolewa Novemba 18, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Camilla Dannevig, wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy.

Bi. Dannevig ameipongeza REA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Norway, akieleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma ya umeme kwenye vitongoji pamoja na mradi wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa, Mha. Saidy ameishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano na ufadhili wake, akibainisha kuwa uwekezaji huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Amesema REA itaendelea kuongeza kasi ya uunganishaji wa wateja wapya sambamba na kuimarisha kampeni za uhamasishaji ili wananchi watumie umeme katika shughuli za uzalishaji mali, biashara na matumizi ya nyumbani pamoja na nishati safi ya kupikia.
Amefafanua kuwa kupitia programu ya kuhamasisha matumizi yenye tija ya umeme (PUE) na nishati safi ya kupikia, REA imetekeleza kampeni ya nyumba kwa nyumba iliyolenga kaya 19,700, ambapo kaya zote zimefikiwa na kuhamasishwa kuunganishiwa umeme.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi wa REA, Mha. Deogratius Nagu, amesema utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme umefikia asilimia 93, huku mradi wa uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia ukifikia asilimia 95.
Mradi wa kusambaza umeme unatekelezwa na Mkandarasi M/s Derm Group (T) Ltd, huku mradi wa uhamasishaji ukitekelezwa na M/s Dar Merchant Group.