Binti Angel Wariaeli (13), aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufuatia kujeruhiwa kwa risasi Oktoba 29, 2025 maeneo ya nyumbani kwao Manzese, Dar es Salaam, amefariki dunia.
Taarifa za kifo cha binti huyo zimethibitishwa leo, Novemba 18, 2026, na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Irene Charles Mbonde, pamoja na taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imewasilisha masikitiko yake kufuatia msiba huo uliogusa jamii na Watanzania wengi waliokuwa wakifuatilia afya yake.
Katika taarifa rasmi kwa waandishi wa habari, uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ulitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huo, ikiwaombea nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.
Angel, ambaye alikuwa ametoka kuhitimu darasa la saba na kujiandaa kujiunga na kidato cha kwanza akiwa na ndoto ya kuwa daktari, alipatwa na mkasa huo mnamo Oktoba 29, 2025, majira ya saa tisa mchana. Tukio hilo lilitokea maeneo ya nyumbani kwao Manzese alipokwenda kumpelekea dada yake simu kwenye kibanda cha chakula cha familia, ambapo alisikia watu wakikimbia na kisha akapigwa risasi ya bega iliyomwangusha chini.
Risasi hiyo iliharibu uti wake wa mgongo na kumfanya ashindwe kutembea au kuendelea na masomo, huku akibaki kulala kitandani na kupata vidonda vilivyolazimu asafishwe hospitalini kila siku ya Ijumaa.
Mnamo Oktoba 31, 2026, taarifa za mahangaiko ya Angel na mama yake mzazi ziliripotiwa na vyombo vya habari ikiwamo The Chanzo, ambapo waliomba msaada wa matibabu kufuatia hali yake iliyomsababisha kukatisha masomo. Kufuatia taarifa hiyo, alipatiwa msaada na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alianziwa matibabu na madaktari bingwa hadi mauti yalipomkuta.