Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi mkoani Morogoro Novemba 22 mwaka huu, ambapo atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akizungumzia ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema kuwa Waziri Mkuu atatumia ziara hiyo kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kupata nafasi ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.
Sendiga amewataka viongozi wa Halmashauri pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kiusalama ili ziara hiyo ifanyike kwa utulivu na bila changamoto zozote.
Aidha, amewahimiza wananchi wa mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika mikutano itakayofanyika wakati wa ziara hiyo ili kupata fursa ya kuwasilisha kero na changamoto zao moja kwa moja kwa Waziri Mkuu.