Mtoto wa miaka 9, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kasota, kijiji cha Kasota, Kata ya Bugulula, halmashauri ya wilaya ya Geita amelazwa hospitalini baada ya tukio la kusikitisha la kuchomwa moto na mama yake mzazi kwa jina la Devota Nestory, miaka 40, Mzinza, Msusi, ambaye alimtuhumu mtoto wake kuiba shilingi 800.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Siwema Kulwa, mama mdogo wa mtoto huyo, tukio hilo lilitokea baada ya majibizano kati ya mtoto na mama yake, ambapo mama huyo alimwaga mafuta ya petroli mwilini mwa mtoto kisha kumchoma moto.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Geita, Dkt. Shadrack Omega amethibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa na majeraha makubwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wake, na kueleza kuwa mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu na kwamba hali yake inaendelea kufuatiliwa kwa ukaribu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, SACP Sophia Jongo amethibitisha kumkamata mama mzazi wa mtoto huyo kwa uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo, ambapo amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu wanaoendelea kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuacha mara moja, kwani halitasita kuchukua hatua kali za kisheria. Aidha, linawasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia, kufichua na kuchukua hatua za haraka dhidi ya vitendo vya ukatili ili kukomesha vitendo hivyo kwenye jamii.