Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini Tanzania tarehe 19 Machi 2025 limefanya maadhimisho ya miaka 72 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1953 kwa kutembelea na kutoa misaada mbalimbali kwenye kituo cha watoto wenye ulemavu cha Mlali kilichopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Kaimu Msajili wa Baraza hilo Bi. Irene Chilewa amesema katika kipindi hicho Baraza hilo limepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wauguzi na wakunga waliosajiliwa wakiwa na madaraja mbalimbali ya elimu mpaka kufikia ngazi ya Uzamivu (PhD) ambao jumla yao wamefikia takribani 54,000, tofauti na miaka 72 iliyopita. Baraza hilo pia linajivunia kujenga mfumo wa TEHAMA, ujenzi wa ofisi zake Kibaha mkoani Pwani na ujenzi wa ofisi unaoendelea Jijini Dodoma.
“katika kuadhimisha siku ya baraza tumekuwa tukitoa misaada na vitu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii ambapo leo tumeleta mahitaji ya watoto yenye thamani ya Shilingi milioni tano”, amesema Bi. Irene.
Kwa upande wake Padri. Gaudence Aikaruwa, ambaye ni Mkurugenzi wa kituo hicho chenye watoto zaidi ya 40 pamoja na kutaja changamoto wanazokumbana nazo katika malezi ya watoto hao ameshukuru msaada huo akiomba taasisi na watu wengine binafsi kuwa na utamaduni wa kuwakumbuka na kuwasaidia wenye uhitaji kwani hakuna aliyependa kuishi kwenye maisha ya ulemavu au maisha duni.
Ikumbukwe kuwa, Baraza la Uuguzi na Ukunga ni mamlaka ya kisheria inayosimamia wanataaluma na taaluma za uuguzi na ukunga Tanzania, chini ya Sheria ya Mwaka 2010 (The Nursing and Midwifery Act, 2010) ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na wauguzi na wakunga nchini Tanzania ni za kiwango kinachokubalika na salama kwa jamii.