Latest Posts

BENKI YA BIASHARA TANZANIA (TCB) YAJITOLEA KUSAIDIA UKUAJI WA TASNIA YA FILAMU NA SANAA NCHINI

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeshiriki katika kikao kazi cha uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania, ambalo linatarajiwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu, ambalo limeandaliwa na taasisi ya Foundation Ambassadors Gender Development Initiatives (FAGDI) kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.

Tamasha hili linawaleta pamoja wadau wa filamu na sanaa, pamoja na wadau kutoka sekta mbalimbali katika jukwaa moja la kujadili mustakabali wa maendeleo ya sekta hiyo kitaifa na kimataifa, changamoto zinazoikabili tasnia ya filamu na kujadili mipango endelevu ya kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Benki ya Biashara Tanzania, Bi. Janeth Zoya, Meneja Mkuu wa Kitengo cha Masoko, alielezea umuhimu wa tamasha hilo kwa kusema,

“Benki ya TCB tunatambua nguvu iliyo nayo sanaa katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Sanaa ni zaidi ya burudani; ni chanzo cha kukuza uchumi, kuchochea umoja wa kitaifa, na kutambulisha utamaduni wetu duniani. Tasnia ya filamu na sanaa ina uwezo mkubwa wa kutuvusha nje ya mipaka, kusimulia hadithi na urithi wetu, na kuonesha ufahari wa tamaduni za Kitanzania duniani.”

Bi. Zoya aliendelea kusisitiza umuhimu wa tamasha hilo kwa kusema kuwa litatoa fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili mikakati itakayokuza uchumi na maendeleo ya sekta hii.

“Ni muhimu kutumia fursa hii kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta, zikiwemo zile zinazohusiana na uwezeshwaji, uelimishaji, na upatikanaji wa masoko. Zaidi ya yote, tunapaswa kutambua fursa zilizopo mbele yetu – uwezekano wa kufanya ushirikiano kimataifa, matumizi ya majukwaa ya kidigitali ili kuifikia hadhara ya kimataifa, na kutengeneza muundo endelevu utakaowezesha mafanikio ya muda mrefu”, ameeleza Bi. Zoya.

Udhamini wa Benki ya TCB katika uzinduzi huu unaimarisha dhamira yake ya kusaidia miradi mbalimbali inayochangia maendeleo ya utamaduni na uchumi nchini. Benki ya TCB inajitolea kuchangia katika kukuza sanaa bunifu na maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla, lengo likiwa ni kuchangia uanzishwaji wa sekta mahiri ya sanaa na utamaduni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!