Mkurugenzi wa Nsong’wa Traditional Clinic Dkt. Damaki Magina, amesema ipo haja ya kujali afya za jamii pasipo kubagua wala kuchagua rika au makundi ya watu, ndio maana wameamua kutoa misaada ya kiafya itakayowasaidia watoto kujilinda katika changamoto mbalimbali za maradhi. Dkt. Damaki ameyasema hayo Aprili 17, 2024 wakati akitoa msaada kwa watoto yatima wanaoishi katika mazingira magumu katika kituo cha Faraja Orphanage kilichopo Mburahati, Dar es Salaam. “Tumeleta vitu vingi kwa ujumla, lengo likiwa ni kuwalinda watoto wasiweze kuingia katika changamoto za maradhi kwa sababu watoto ni wengi na wanakaa pamoja, hatusubiri mtu au mtoto aumwe ndipo tuwahudumie, tunawahudumia kabla hawajapata changamoto kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba” Amesema Dkt. Damaki. Akipokea msaada huo Bi Zamda Juma ambaye ni msimamizi kituoni hapo ametoa shukrani kwa Taasisi ya Nsong’wa Tradition Clinic kwa msaada huo huku akitoa rai kwa wadau wengine kuwasaidia kupata bima za afya ambazo ni changamoto kwa watoto wanaoishi kituoni hapo.