Latest Posts

CBE YAJA NA MTAALA KUFUNDISHA PHD YA INFOMATIKI ZA BIASHARA

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kinatarajia kuanzisha programu ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Infomatiki ya Biashara ili kuleta mabadiliko ya uchumi wa kidijiti na teknolojia katika kufanya biashara za kidijiti kuendana na mabadiliko ya dunia.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kujadili mtaala wa masomo hayo yaliyowashirkisha wataalamu wabobezi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

Wataalamu hao walikuwa wakipitia mtaala ambao umeandaliwa na chuo hicho na kutoa maoni yao ili baada ya hapo upelekwe kwa mdhibiti ambaye ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTIVET) kwaajili ya kupewa ithibati na kuanza kutumika.

Wataalamu wa vyuo vikuu wakipitia mtaala wa infomatiki za biashara unaotarajiwa kuanzishwa na Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam CBE

Amesema kuanzishwa kwa shahada hiyo ni hatua muhimu yenye kuleta mabadiliko katika kuendeleza elimu ya juu, kukuza uvumbuzi wa kiteknolojia na kuchangia ajenda ya maendeleo ya taifa.

Amesema CBE ambayo ina kampasi nne nchini kwa muda mrefu imekuwa kinara katika kutoa programu mbalimbali za kitaaluma, na kwa kushirikana na Chuo Kikuu cha Ufini ya Mashariki kimeandaa mtaala wa infomatiki za biashara.

Amesema Shahada ya PhD kwenye infomatiki za biashara ni muhimu kwani inachanganya utaalamu wa biashara na uvumbuzi wa kiteknolojia ikilenga uchanganuzi wa data, mifumo ya habari, mabadiliko ya dijiti na utafiti unaotegemea suluhisho.

“Wahitimu wa program hii wanatafutwa sana kwenye sekta ya umma na binafsi na watakuwa wahusika wakuu katika kuleta mabadiliko ya teknolojia katika tasnia mbalimbali nchini,” amesema.

Aidha Profesa Lwoga amesema mtaala huo utawapa wanafunzi wa Tanzania ujuzi unaohitajika ili kuendesha na kuongoza katika uchumi wa kidijiti na kuchangia katika uboreshaji wa maendeleo ya viwanda.

Amesema mtaala huo utasaidia kuongeza tija katika biashara za kidijiti na kuimarisha ushindani wa kimataifa pamoja na kuongeza ujuzi katika kufanya tafiti na uvumbuzi wa kiteknolojia katika sekta ya biashara za kidijiti

“Mkutano huu ni muhimu katika kuunda mustakabali wa programu hii na maoni yenu wadau yatasaidia kuunda mtaala unaoakisi mahitaji ya soko la ajira na kuendana na malengo ya maendeleo Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa wanatarajia baada ya kupata ithibati, mtaala huo utaanza kutumika hapa nchini na utakuwa mtaala wa kwanza kwenye biashara ya infomatiki ambao utaenda kuzalisha wataalamu watakaokuwa watafiti wabobezi katika uvumbuzi wa kiteknolojia na kuangalia mifumo itakayosaidia kwenye biashara.

“Hivi sasa teknolojia inabadilika kwa haraka sana na kuna Akili Mnemba (AI) yote tumeyazingatia kwenye huo mtaala na juhudi kama hizi tulianza mwaka 2014 ambapo tuliingia makubaliano na chuo cha Finland Mashariki ambao wanatoa program hii muda mrefu,” amesema na kuongeza,

“Walitusaidia sana kuwapa mafunzo wataalamu wetu ambao tumekuwa tukiwapeleka kwenye chuo hicho na mpaka sasa tuna walimu wengi ambao wameshahitimu kwenye shahada ya infomatiki ya biashara Finland, na sita bado wanaendelea na masomo yao huko huko,” alisema

Angela Runyoro, Mhadhiri Mwandalizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), amesema mitaala hiyo itawezesha kuwafundisha watu kutoka ndani na nje ya nchi kupata ujuzi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika biashara.

“Kwa sasa TEHAMA inahitajika katika sekta zote, hakuna namna unaweza kufanya jambo ukaikwepa na CBE wenyewe wamejikita kuanza kutengeneza wataalamu wa infomatiki za biashara kwa kujua mifumo ya kuendesha biashara kisasa,” amesema Runyoro na kuongeza,

“Hawa wataalamu watafundisha, wengine watafanya tafiti, watachambua mifumo inayofaa katika teknolojia ya kustawisha biashara ili watu wasifanye biashara kizamani. Hii itakuwa na manufaa sana kwa wafanyabaishara na nchi na ulimwengu kwa ujumla”.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!