Wakati tukielekea kwenye hatua ya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, uteuzi ambao unatarajiwa kutangazwa na mamlaka inayoratibu na kusimamia uchaguzi huo (OR-TAMISEMI) kumekuwa na minong’ono kuhusiana na wagombea wa vyama vya upinzani nchini
Hadi sasa imeshuhudiwa viongozi wengi wa vyama vya upinzani nchini hususani vyama vikuu viwili (2) vya CHADEMA na ACT Wazalendo wakijitokeza hadharani na kudai kuwa wagombea wao wamekuwa wakiandaliwa njama ili waweze kuenguliwa katika mchakato huo, ambapo wanadai kuwa mpango huo unalenga kurahisisha njia kwa wagombea wa CCM kwenye vitongoji, vijiji na mitaa
Jambo TV imepata taarifa fiche kutoka ndani ya baadhi ya vyama vya upinzani nchini ikida kuwa vyama hivyo vimesimamisha wagombea wachache kuliko uhalisia unavyosemwa, na kwamba inadaiwa kuwa kinachofanyika kwa sasa ni viongozi wa vyama hivyo kutengeneza ajenda ya kuuamisha umma kuwa wamesimamisha wagombea wengi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili pale uteuzi rasmi utakapotangazwa Ijumaa hii ya Novemba 08.2024 ajenda hiyo iwe imekamilika
Hiyo ikimaanisha kwamba wakati uteuzi wa wagombea hao unafanyika na endapo vyama vya upinzani havijasimamisha wagombea kama inavyodaiwa, basi ni dhahiri majina ya wagombea wa upinzani yatakayotangazwa kuwa yamepitishwa yatakuwa machache jambo ambalo litachochea umma kurejea taarifa za awali za vyama hivyo na kisha kukubaliana na hoja kuwa wagombea hao watakuwa wameenguliwa kwa hila za serikali, TAMISEMI na serikali kwa ujumla wake jambo ambalo si sahihi
Baada ya kupokea madai hayo Jambo TV imemtafuta Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika ambaye hakutoa takwimu za moja kwa moja za idadi ya wagombea waliosimamishwa na chama hicho badala yake ameeleza kuwa viongozi wote wa CHADEMA kanda nchini wametoa orodha na takwimu za wagombea wa chama hicho waliosimamishwa kwenye maeneo yao
Sambamba na hilo, Mnyika alienda mbali zaidi na kueleza kuwa CHADEMA ngazi ya Taifa itatoa taarifa yake kwa wanahabari kuhusiana na zoezi hilo hivi karibuni
Katika kudhihirisha jambo hilo, mapema leo, Alhamisi Novemba 07.2024 akiwa kwenye mafunzo ya wagombea wa CHADEMA mkoa wa Dar es Salaam, Katibu wa chama hicho Kanda ya Pwani Jerry Kerenge amesema katika mkoa wa Dar es Salaam wenye mitaa 564, na kwamba hadi kufikia Novemba 01.2024 saa 10 jioni ofisi yake ilipokea taarifa kuwa CHADEMA imefanikiwa kusimamisha mitaa 547 ambapo ni sawa na asilimia 95 ya mitaa yote, jambo ambalo aamesema hatua hiyo inaonesha kwamba chama hicho kiko tayari kushinda mitaa yote
Aidha, Jerry amesema katika wajumbe 3427 wanaohitajika chama hicho kimeweka wajumbe 3218 sawa na asilimia 98 ya wajumbe wote, huku akitumia nafasi hiyo kujigamba kuwa baada ya Novemba 27.2024 CHADEMA itakuwa inaongoza asilimia 95 ya mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam
Kama hiyo haitoshi, Jambo TV imezungumza pia na Naibu Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Shangwe Ayo ambaye ameeleza kuwa chama hicho kimesimamisha wagombea zaidi ya asilimia 50 nchini kote
Alipoulizwa ni kwa nini hawajasimamisha wagombea kwa asilimia 100 kama walivyojinasibu hapo awali wakati wa kuanza kwa mchakato huo, Shangwe amejibu kuwa anapozungumzia asilimia zaidi ya 50 tafsiri yake ni kwamba inaweza kuwa asilimia 60, 70 nk, hivyo kutumia nafasi hiyo kutoa shukrani na pongezi kwa wanachana wa chama hicho nchini kote
Amesema ni jambo ambalo linaleta faraja kubwa kuona chama cha siasa chenye umri usiozidi miaka 10 kina uwezo wa kusimamisha wagombea karibu kwenye kila jimbo, suala ambalo amedai kuwa baadhi ya vyama vya siasa vimeshindwa kufanya hivyo licha ya uwepo wake hapa nchini kwa muda mrefu
Maswali ya msingi yanayochochea mjadala huu ni kwamba kwa ujumla wake na pengine kuondoa sintofahamu iliyopo ni kwamba, vyama vya upinzani ikiwemo CHADEMA na ACT Wazalendo vinapaswa kuweka wazi kwa takwimu kuwa vilisimamisha wagombea wangapi kwenye vitongoji, vijiji na mitaa?, na je ni vitongoji, vijiji na mitaa mingapi ambayo hawajafanikisha kuweka wagombea na kwa nini?
Lakini pia wanapaswa kuweka wazi kwa takwimu na pengine kwa majina halisi ni wagombea wangapi wameenguliwa au kufanyiwa figisu kwa namna moja au nyingine?, na je kati ya hao ni wangapi wamekuwa wasaliti na wangapi wamesimama imara ambao wamegoma kurubuniwa?
Majibu ya maswali hayo na mengine yanayofanana na hayo yatatoa mwangaza wa suala hilo, lakini kwa sasa kinachosubiriwa ni hatma ya wagombea wote kuona nani na nani au wa wapi ambaye ameteuliwa kugombea, hatua ambayo inapaswa kutekelezwa na mamlaka ya usimamizi wa uchaguzi.