Latest Posts

CHADEMA SONGWE YALIA NA MAISHA KUWA MAGUMU NA DENI LA TAIFA KUPAA

Na Josea Sinkala, Songwe.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa kimesema utitiri wa kodi na hali ngumu ya maisha kwa wananchi vimesababishwa na sera mbovu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Nyasa Frank Mwakajoka wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Vwawa mjini mkoani Songwe.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo, mahali pengi bado maji ni shida katika nchi hii, na mtakumbuka ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG) ni wizi mtupu na hatujaona wahusika wakikamatwa na kuchukuliwa hatua”, Amesisitiza Mwakajoka.

Aidha kiongozi huyo amesema Tanzania imejaa kodi na tozo mbalimbali sanjari na madeni akidai deni la Taifa mpaka sasa halipungui Shilingi billioni tisini licha ya serikali kueleza kuwa deni hilo ni himilivu.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Songwe Isakwisa Lupembe amesema CHADEMA itaendelea kuwa imara katika kuwatetea wananchi na kwenda kushika dola baadaye na kuwatolea uvivu wanaodai Mchungaji Peter Msigwa ameondoka na watu kwenda CCM kwamba CHADEMA ni taasisi isiyoyumba kwa nafsi ya mtu mmoja.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Vwawa Mchungaji Amoni Mwashitete, amesema CHADEMA imejipanga katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu kuhakikisha inashinda hivyo amezindua mkutano huo ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya hadhara katika jimbo lote la Vwawa kutoa elimu ya uraia kuhakikisha wananchi wanajitokeza kujiandikisha na kuchagua viongozi bora chaguzi zijazo.

Naye mwanaharakati Mdude Nyagali Mpaluka (Mdude Chadema) ameeleza kukerwa na ufujaji fedha za umma kukithiri kwa wizi na kutoa onyo kwa watakaohujumu chaguzi zijazo.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!