Wakazi wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam wako hatua chache kupunguza kwa kiwango kikubwa gharama za uondoshaji na usimamizi wa majitaka, kufuatia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kukamilisha ujenzi wa mitambo miwili midogo ya kisasa ya kuchakata majitaka katika Kata za Vijibweni na Gezaulole, inayohudumia wakazi zaidi ya 410,400.
Mitambo hiyo, iliyogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.3, imejengwa maalum kwa ajili ya kuchakata majitaka yanayozalishwa katika maeneo hayo, pamoja na kutoa huduma kwa malori na magari yanayojihusisha na shughuli za uondoshaji majitaka ndani ya Wilaya ya Kigamboni.

Meneja wa Miradi ya Majitaka wa DAWASA, Mhandisi Eric Mutalemwa, amesema kuwa mitambo hiyo imekamilika kikamilifu, imefanyiwa ukaguzi wote wa kitaalamu, na sasa ipo tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
“Miradi hii ya Vijibweni na Gezaulole ni ya kisasa ya kuchakata majitaka. Tumekagua na kujiridhisha na ukamilishaji wake na sasa iko tayari kutumika kuhudumia wananchi na watumiaji wa magari ya uondoshaji majitaka katika Wilaya hii,” amesema Mhandisi Mutalemwa.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza mzigo mkubwa wa gharama ambazo watoa huduma binafsi na wananchi walikuwa wakizipata wakati wa kusafirisha majitaka hadi kwenye mabwawa ya mbali.
Mtazamo huo umeidhinishwa na madereva wa malori ya majitaka eneo hilo, akiwemo Habibu Ally, aliyeeleza kuwa mradi huo utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji kwa kuwa hautalazimu tena kusafiri umbali mrefu hadi Vingunguti au Kurasini.
“Awali ilitulazimu kwenda hadi katika mabwawa ya majitaka Vingunguti na Kurasini. Umbali huo ulifanya tozo kuwa kubwa kwa wateja na kuongeza gharama za uendeshaji wa magari. Mitambo hii itatusaidia kumwaga majitaka hapa hapa Kigamboni na kutupunguzia gharama,” amesema Ally.
Hatua hii inaelezwa kuongeza tija kubwa katika uboreshaji wa usafi wa mazingira wilayani humo na kurahisisha huduma za kijamii kwa ufanisi zaidi.
