Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Hamad Mbega, amefanya ziara maalum katika eneo la kihistoria la Kimondo lililopo wilayani humo ikiwa ni mwendelezo wa ziara wa kutembelea taasisi za umma wilayani humo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbega amebainisha kuwa eneo la Kimondo ni urithi wa thamani kwa Taifa na lina nafasi kubwa katika kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha eneo hilo linaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Mbega ametoa wito kwa jamii inayozunguka eneo hilo kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi katika kulinda na kutunza kivutio hicho.
Kimondo cha Mbozi ni moja ya kimondo kikubwa Duniani na kufanya kuwa kivutio cha kipekee kwa wanasayansi, wanahistoria na watalii, mamlaka ya Ngorongoro, inayosimamia eneo hilo, imeweka juhudi kubwa kuhakikisha urithi huo unaendelea kuwa kivutio cha kimataifa.
Mbega amesisitiza kuendelea kuhifadhi mazingira na uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda urithi wa taifa.
Sanjari na hayo ameahidi kushirikiana na mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza ili kuboresha uzoefu wa watalii na kuongeza mapato ya wilaya na Taifa kwa kwa ujumla
Aidha, ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Ngorongoro kwa kazi nzuri ya kusimamia eneo hilo na kuhakikisha linaendelea kuwa salama.
Wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alikutana na watumishi wa eneo hilo na baadhi ya viongozi wa kata ya Mlangali na kuzungumza nao kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha eneo hilo na kuongeza idadi ya watalii na kuhifadhi mazingira.
Pia, amewahimiza wananchi kuona umuhimu wa utalii kama moja ya njia za kuimarisha maisha yao kupitia fursa za ajira na biashara katika maisha yao ya kila siku.