Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limethibitisha kumkamata Shadrack Michael Swai (37), mkazi wa Arusha, ambaye ni dereva wa basi lenye namba za usajili T-458 DYD aina ya YUTONG, mali ya kampuni ya Asante Rabi. Dereva huyo anatuhumiwa kusababisha ajali mbaya iliyotokea wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, na kusababisha vifo vya watu nane na kujeruhi wengine 39.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alithibitisha kukamatwa kwa dereva Swai jioni ya Oktoba 22, 2024, baada ya dereva huyo kutoroka mara baada ya ajali kutokea.
“Swai anakabiliwa na kosa la kuendesha gari kwa uzembe, kushindwa kuchukua tahadhari, na kusababisha ajali iliyopelekea vifo na majeruhi,” amesema DCP Mutafungwa.
Ajali hiyo ilitokea Oktoba 22, 2024, majira ya saa 6:10 asubuhi, katika kijiji cha Ngudama, wilayani Misungwi, kwenye barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga. Gari la kampuni ya Asante Rabi, likiendeshwa na Swai, lilihama upande wake wa barabara na kugongana uso kwa uso na basi jingine aina ya YUTONG lenye namba T-281 EFG, mali ya kampuni ya Nyehunge, ambalo lilikuwa linatokea Morogoro kuelekea Mwanza.
Kamanda Mutafungwa ameeleza kuwa ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu nane, ambapo watano walifariki papo hapo kwenye eneo la tukio, na wengine watatu walifariki dunia walipokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Misungwi. Miongoni mwa waliofariki, wanne wametambuliwa kama Zamda Darius (30) mkazi wa Usagara, Jacob Elius (43) mkazi wa Chibe Shinyanga, Godluck Mshana (18), na Edward Lazaro (20) mkazi wa Shirati. Miili ya watu wanne ambao bado hawajatambulika imehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Misungwi.
Majeruhi waliopo hospitali ya Rufaa ya Bugando ni Doricas Joseph (38), Shija Kazori (41), Magreth Hardson (31), Isack Daud (28), Amani Andrew (27), Silivia Sita (28), na Janeth Mathias (26).