Latest Posts

DKT. KIKWETE MGENI RASMI KONGAMANO LA KUMBUKIZI YA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE KIBAHA

 

Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kimataifa la kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kongamano hilo la siku moja litafanyika kesho, Oktoba 11, 2024, katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.

Akizungumza na gazeti la Uhuru, Mkuu wa Shule ya Uongozi, Profesa Marcelina Chijoriga, alisema kongamano hilo litawaleta pamoja wageni mashuhuri wakiwemo Mkuu wa Majeshi wa Zimbabwe, Luteni Jenerali Anselem Sanyatwe, na Naibu Balozi wa China nchini Tanzania, Suo Peng. Watawasilisha mada zao katika kongamano hilo, ambalo limeandaliwa kwa lengo la kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere katika harakati za ukombozi wa Afrika.

Jenerali Sanyatwe atatoa mada kuhusu “Changamoto na Fursa za Kuendeleza Dira ya Nyerere: Mtazamo kutoka kwa Vyama Rafiki Sita,” huku Naibu Balozi Peng akiwakilisha Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa kuzungumzia “Ujenzi wa Madaraja: Alama Isiyofutika ya Msaada wa Mwalimu Nyerere kwa Vyama vya Ukombozi na Uhusiano wa Afrika na Dunia.” Rais mstaafu Kikwete atafungua rasmi kongamano hilo.

Kwa mujibu wa Profesa Chijoriga, wazungumzaji wengine kutoka nchi mbalimbali kama Namibia, Zimbabwe, China, na Tanzania watashiriki, huku Kanali mstaafu wa JWTZ, Joseph Simbakalia, akitoa mada kuhusu “Jukumu la Mwalimu Nyerere katika Mapambano ya Ukombozi wa Afrika.” Dkt. Charles Mubita, Mjumbe wa Kamati Kuu ya SWAPO nchini Namibia, pia atatoa mada kuhusu “Jukumu la Elimu ya Itikadi katika Kuhifadhi Alama ya Nyerere.”

Kongamano hilo linaandaliwa kwa uamuzi wa Bodi ya Usimamizi ya Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, ambayo ina wawakilishi kutoka vyama rafiki vya MPLA (Angola), CCM (Tanzania), SWAPO (Namibia), ZANU PF (Zimbabwe), ANC (Afrika Kusini), FRELIMO (Msumbiji), na CPC (China). Lengo ni kumuenzi Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa kiongozi wa kimataifa, na kuhakikisha historia yake inawafikia vijana wa sasa.

Profesa Chijoriga aliongeza kuwa zaidi ya wageni 200 kutoka nchi mbalimbali wamesha thibitisha kushiriki, wakiwemo kutoka Afrika Kusini, China, Msumbiji, Angola, na nchi nyingine za Afrika, pamoja na Umoja wa Afrika (AU). Mwanasiasa mkongwe Stephen Wassira pia atatoa mada kuhusu “Maono ya Mwalimu Nyerere juu ya Kujitegemea Kiuchumi kwa Afrika.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!