Siku chache baada ya Jambo TV kutoa taarifa za uwepo wa madai ya mamia ya watu kutoka maeneo tofauti nchini wanaodai kutapeliwa na kampuni ya ‘Pig Investment International’ (Kijiji cha Nguruwe) inayoongozwa na Mkurugenzi wake Simon Mkondya (Dr. Manguruwe), huku wakiomba serikali kuingilia kati suala hilo, hatimaye mfanyabiashara huyo amefikishwa Mahakamani leo, Jumanne Novemba 05.2024
Dr. Manguruwe mwenye umri wa miaka 40 ambaye pia ni Mkurugenzi wa iliyokuwa kampuni ya ‘Vanilla International Ltd’ amefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam sambamba na aliyekuwa mfanyakazi wake kwenye kampuni ya Vanilla International Ltd Rweymamu Joh mwenye umri wa miaka 59 ambaye inaelezwa kuwa wakati huo alikuwa mkaguzi wa kampuni hiyo
Wakiwa Mahakamani hapo wawili hao wamesomewa mashtaka 28 ikiwemo mashtaka ya utakatishaji wa fedha wa zaidi ya shilingi milioni 90 za Kitanzania, ambapo kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema amesema watuhumiwa wametenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Januari mosi mwaka 2020 na Desemba mosi mwaka 2023 kwenye maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aaron Lyamuya imeelezwa kuwa katika mashtaka hayo 19 ni ya kufanya biashara ya upatu ambapo inadaiwa kuwa katika kipindi hicho Dr. Manguruwe na mwenzake walifanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu kulingana na kiasi cha fedha watakachowekeza
Katika muktadha huo, inadaiwa kuwa washtakitwa hao wawili walijipatia jumla ya shilingi za Kitanzania milioni 92.2 kutoka kwa watu 19 tofauti ambapo watu hao walitoa kiasi cha fedha tofauti kila mmoja, lakini wote kwa nyakati tofauti waliahidiwa kwamba wangepata faida mara mbili au tatu ya fedha walizowekeza
Imeendelea kudaiwa Mahakamani hapo kuwa, mashtaka tisa ni ya utakatishaji ambayo yanamkabili Dr. Manguruwe pekee ambapo pia inaelezwa kuwa alijipatia viwanja tisa kitalu namba AB eneo la Idunda, mkoani Njombe, huku ikielezwa kuwa alifanya yote hayo huku akijuwa wazi kwamba viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya upatu
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema amedai Mahakamani hapo kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hivyo washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote
Kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka washtakiwa hao wamekosa dhamana, hivyo wamerejeshwa ‘gerezani’ huku shauri hilo likihairishwa hadi Novemba 19.2024 kwa ajili ya kutajwa tena.