Viongozi wametakiwa kuhakikisha haki inazingatiwa katika kusimamia na kutekeleza utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu ili kuwezesha maendeleo endelevu kwa wananchi.
Wito huo ulitolewa Novemba 25, 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati wa mafunzo kwa viongozi kuhusu urejeshwaji wa mikopo ya vikundi vya jamii yaliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mpogolo aliwahimiza viongozi kuhakikisha walengwa wa mikopo wanazingatiwa, hususan vikundi vilivyoundwa rasmi ambavyo vina uwezo wa kutumia mikopo hiyo kubadilisha maisha yao. Aidha, amewataka viongozi kupokea mapendekezo kutoka kwa jamii na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa mikopo na kuleta maendeleo katika Wilaya ya Ilala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amewahimiza viongozi kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kuchukua mikopo hiyo. Amesema juhudi za viongozi katika kusambaza elimu ya mikopo zitawasaidia wananchi kuelewa umuhimu wa mikopo hiyo na namna ya kuitumia kwa maendeleo ya kiuchumi.
Mabelya pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hiyo, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Katika mafunzo hayo, viongozi waliapishwa kulingana na vyeo vyao na majukumu yao, ambapo waligawanywa katika makundi matatu: menejimenti, kamati ya huduma ya mikopo, na kamati ya uhakiki kwa ngazi ya wilaya.