Takriban watu 125 wameuawa nchini Msumbiji katika siku tatu za ghasia za nchi nzima, wakati wa maandamano yaliyoongozwa na upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, shirika lisilo la kiserikali Plataforma Decide liliripoti Alhamisi. Ripoti hiyo pia inaongeza idadi ya jumla ya vifo kufikia 252 tangu ghasia zilipoanza mwezi Oktoba.
Kiongozi mkuu wa upinzani, Venansio Mondlane, ameshutumu vikosi vya usalama kwa kuchochea ghasia na kuhusika katika wizi wa ngawira, akidai kuwa lengo ni kuruhusu chama tawala, Frelimo, kutangaza hali ya dharura baada ya uchaguzi uliojaa utata.
Mahakama ya juu nchini Msumbiji ilithibitisha wiki hii ushindi wa chama cha Frelimo katika uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 9. Chama hicho, ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Ureno mwaka 1975, kilitangaza kuwa mgombea wake, Daniel Chapo, alipata ushindi wa asilimia 65.17 ya kura.
Hata hivyo, mpinzani mkuu wa Chapo, Venansio Mondlane, amedai kuwa uchaguzi huo uliibwa. Mondlane alitangaza wazi nia yake ya kuchukua madaraka, hali iliyochochea maandamano ya nchi nzima na kusababisha wiki kadhaa za machafuko.
Maandamano hayo yamesababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na mauaji na uvunjaji wa jela ambapo wafungwa takriban 1,000 walitoroka.
Mondlane ameshutumu vikosi vya usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kuruhusu wizi wa mali za umma. Alidai kuwa hatua hizo zinalenga kuhalalisha kutangazwa kwa hali ya dharura ili kudhibiti upinzani na kuimarisha utawala wa Frelimo.
“Vikosi vya usalama vimechochea ghasia na wizi wa mali ili kuhalalisha hali ya dharura,” Mondlane alisema, akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kurejesha haki na utulivu nchini.
Ghasia hizi zimeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa amani na demokrasia nchini Msumbiji. Katika historia yake, Frelimo limekuwa na uhusiano wa mvutano na vyama vya upinzani, huku nchi hiyo ikikabiliana na changamoto za kisiasa na kiusalama, ikiwemo uasi wa kijeshi na mgogoro wa kiuchumi.
Huku ghasia zikiendelea, jamii ya kimataifa imeitaka serikali ya Msumbiji na vyama vya upinzani kushirikiana kutafuta suluhisho la amani kwa mgogoro huu, huku ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu demokrasia na haki za binadamu.