Latest Posts

HALMASHAURI ZATAKIWA KUANDAA MWONGOZO WA MAADILI KWA BAA NA KLABU KUZUIA UKATILI WA KIJINSIA

Halmashauri nchini zimehimizwa kuandaa mwongozo maalumu wa maadili kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa baa na klabu katika maeneo yao, ili kuepusha vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana vinavyotokea katika sehemu hizo za starehe.

Pendekezo hili ni moja kati ya matano yaliyotolewa na washiriki wa Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya 2024, baada ya majadiliano yaliyohusisha uwajibikaji wa serikali, wadau wa maendeleo, na wanajamii, ikiwemo halmashauri, katika tamasha hilo limefanyika wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.

Akitoa maoni yake wakati wa kilele cha tamasha hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali alisisitiza kuwa ukosefu wa miongozo thabiti kwa wamiliki na wasimamizi wa sehemu za starehe ni moja ya vyanzo vikuu vya mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinsia kwa wanawake.

“Ningependa kusisitiza kuwa baa na klabu zimegeuka na kuwa sehemu za kufanya shughuli za starehe usiku na mchana, hali ambayo si tu kwamba inaharibu maadili, bali pia inakwamisha maendeleo kwa kuathiri usingizi wa watu waliotoka kuzalisha mali mchana kutwa ili kulipa kodi,” alisema Gemma.

Gemma aliongeza kuwa wadau wa tamasha wamependekeza serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na teknolojia za kisasa zinazoweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.

Alisema kwamba bado kuna changamoto kubwa ya umiliki wa ardhi kwa wanawake, ambapo ni takriban asilimia 20 tu ya wanawake ndio wanaomiliki ardhi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika sera za kisekta, sheria, na programu mbalimbali, ikiwemo Sera ya Maji (2002), Sera ya Elimu na Mafunzo (2014), na Sera ya Afya (2007).

“Juhudi hizi zimesaidia katika ongezeko la upatikanaji wa maji kutoka asilimia 50 mwaka 2000 mpaka asilimia 86.7 kwa mwaka 2020 kwa upande wa mijini, wakati upande wa vijijini, imetoka asilimia 55 mwaka 2000 hadi asilimia 72.3 mwaka 2020”, ameeleza Liundi.

Hata hivyo, Lilian aliongeza kuwa licha ya ongezeko la miundombinu, changamoto kubwa bado ni upatikanaji wa maji safi na salama pale yanapohitajika, kwani “bomba si maji,” na upatikanaji wa maji kwa gharama nafuu au bure kabisa bado haujafikiwa ipasavyo.

Lilian pia alifafanua kuwa idadi ya wafanyakazi wanawake katika Wizara ya Maji imeongezeka hadi kufikia asilimia 60 ya wafanyakazi wote, lakini ni asilimia 24 tu ya wanawake hao ndio walio katika ngazi za maamuzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!