Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dodoma inatarajiwa kutoa uamuzi juu ombi la Kanisa la Ufufuo na Uzima (Glory of Christ Tanzania Church) kuweza kuendelea kutoa huduma za kiroho kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya makanisa hayo maeneo mbalimbali nchini kufungiwa.
Hili limakuja baada ya kufunguliwa kwa shauri no.13189 la 2025 lililofunguliwa na kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church, dhidi ya IGP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Taasisi za Kiraia likiitaka mahakama kuondoa zuio la kufungiwa kwa kanisa hilo wakati Rufaa iliyokatwa na Kanisa hilo kupinga kuzuiwa kwa shughuli zake za kidini ikifanyiwa kazi.
Kupitia Wakili wa Kanisa hilo Peter Kibatala akizungumza na Maaskofu na Wachungaji wa waliojitokeza kumsikiliza leo jijini Dodoma ameeleza kuwa ameomba kupewa muda mpaka tarehe 18 ili aweze kupeleka maelezo ya ziada kwa kiapo juu shauri hilo kutokana na mambo yaliyojitokeza yakihusiana na shauri hilo.
Ameongeza kuwa upande wa serikali umepewa muda mpaka tarehe 25 ya mwezi huu kuweza kujibu kiapo cha maelezo ya awali pamoja na maelezo ya ziada ambayo yatatolewa na upande wa utetezi juu ya kwa nini kanisa hilo lisipewe anri ya zuio dhidi ya IGP na wengineo.
Baada ya hapo upande wa utetezi utaujibu upande wa serikali tarehe 30, Juni 2025 na tarehe 08/7/2025 mahakama itatoa maamuzi ya hoja za pande zote baada ya kuzisikiliza.
Moja ya mambo yanayofanya uamuzi huo kusogezwa mpaka Julai ni kile kilichoelezwa na Kibatala kuwa alipokea barua kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwa imesainiwa na Waziri mwenye dhamana Innocent Bashungwa yakuwa barua iliyoenea mitandaoni juni 02 sio sahihi kwani haina sahihi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia.
Waziri wa mambo ya Ndani kupitia barua yake ya Juni 06, aliiarifu ofisi ya Kibatala kuwa rufaa waliyoikata ya kuomba kanisa lisizuiwe kufanya kazi sio sahihi kwani wameeleza kuwa kanisa lilikofungiwa ni la Glory of Christ Church huku usajili ukiwa unaonyesha kanisa lililopo chini ya Askofu Dkt Josephat Gwajima ni la Glory of Christ Tanzania Church.
Pamoja na mambo mengine kibata amehoji jeshi la polisi lilifunga makanisa ya Gwajima kwa kupitia barua ipi?. Huku akihoji je ni ile ambayo haikusainiwa au kuna nyingine ambayo wateja wake hawajaiona?.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima(Glory Of Christ Tanzania Church), Maximilian Machumu Kadutu(Askofu Mwanamapinduzi) ametangaza kuwa kuanzia jumapili hii ya tarehe 22 waumini wa kanisa hilo wataendelea na ibada makanisani kama ilivyokuwa mwanzo kwa kuwa kanisa hilo halijafungiwa.
Mwanamapinduzi amehoji kuwa endapo akikosea Katekista au Padri mmoja wa Kanisa Katoliki je kanisa hilo litafungiwa.
Akizungumza kwa uchungu na waumini hao wakati akiwaaga Wakili Kibatala aliwaasa kuwa imara sana kipindi hiki cha mpito huku akisisitiza wamuombee.