Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Baraza la Wanawake (BAWACHA), Hilda Newton, ameachiwa kwa dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central), jijini Dar es Salaam, baada ya sintofahamu ya zaidi ya saa 12 tangu kupotea kwake.
Hilda alionekana kwa mara ya mwisho katika eneo la Kisutu akiwa miongoni mwa waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa kesi ya mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu, hali ambayo ilizua taharuki na mashaka miongoni mwa wanaharakati na wadau wa haki za binadamu.
Taarifa za kutoweka kwake zilisababisha mashinikizo kutoka kwa viongozi wa chama hicho na watetezi wa haki, hasa baada ya Jeshi la Polisi kutangaza jana kuwa limewaachia watu kadhaa waliokuwa wamekamatwa, huku jina la Hilda likikosekana miongoni mwa waliotajwa.