Latest Posts

HUDUMA ZA MIONZI KITUO CHA CHIWALE KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA MATIBABU NDANDA

Zaidi ya wakazi 50,000 wa Kijiji na Kata ya Chiwale, Jimbo la Ndanda, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara wanatarajiwa kunufaika na mradi wa huduma za mionzi unaoendelea kujengwa katika Kituo cha Afya Chiwale.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi milioni 150 hadi kukamilika kwake, lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya na kupunguza changamoto kwa wagonjwa wa kata hiyo na maeneo jirani.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax, alipotembelea mkoa wa Mtwara kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Waziri Tax ameeleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa viongozi kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Mradi huo wa kituo cha afya unatarajiwa kutoa huduma muhimu kama mionzi, X-ray, na uchunguzi wa magonjwa ya moyo, hususani kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu kutokana na ajali na magonjwa mengine.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe, ameeleza furaha yake kwa kukamilika kwa mradi huo, akisema kuwa sasa wakazi wa Chiwale hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo katika Hospitali ya Ndanda.

Mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Shamsi Hassan, amesema: “Tunaishukuru sana serikali kwa kuleta huduma hii, itatuondolea adha ya kusafiri kwenda hospitali za mbali kutafuta huduma za mionzi.”

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amebainisha kuwa miradi hii ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi. Ameeleza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, mkoa wa Mtwara umepokea zaidi ya Shilingi bilioni 740 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo elimu, maji, barabara, na umeme.

Waziri Tax alihitimisha kwa kusema: “Rais Samia ana nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata maendeleo na changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati.”

Kwa kuimarisha huduma za afya, serikali inatarajia kuboresha hali ya maisha ya wananchi na kupunguza vifo vinavyotokana na upungufu wa huduma za matibabu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!