Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kujitangaza nje ya mipaka ya Tanzania ili kiweze kupata wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.
Amesema badala ya kutegemea wanafunzi wa ndani pekee chuo hicho kina uwezo wa kupata wanafunzi kutoka mataifa mengine kwani taaluma inayotolewa chuoni hapo inakidhi vigezo vya kimataifa.
Ameyasema hayo siku ya Jumatatu Februari 10, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Pia amewataka vijana wasomi nchini kushirikiana na kampuni mbalimbali za uzalishaji kutumia fursa ya ukuaji wa Fursa za Afrika (AGOA) kupeleka bidhaa nyingi kutoka Tanzania kwenye soko la Marekani.
Amesema soko hilo linatoa fursa ya aina 6,500 za bidhaa kuingia Marekani lakini bado halijatumika ipasavyo kuchangia ukuaji wa kipato cha Watanzania na taifa kwa ujumla hivyo kuna umuhimu wa kuchangamka kuzipita nchi zingine.
Amesema chuo cha CBE kina wajibu wa kuandaaa vijana mahiri wanaoweza kushiriki kwenye biashara za kitaifa na kimataifa wakiwa na ujuzi uliokamilika hivyo kumudu kushindana na wenzao kimataifa.
“Nchi yetu imefunguka kimasoko, tunahitaji vijana mahiri wenye ufahamu wa kutosha wa kutumia fursa za masoko zilizopo kufanya biashara za kimataifa. Vijana wakiwa na maarifa wakishirikiana na wazalishaji watauza sana bidhaa nje ya nchi,” amesema na kuongeza,
“Kwenye AGOA tumefanya vizuri lakini tunatakiwa kufanya vizuri zaidi ya hapo na kwenye nchi za Afrika kuna soko kubwa lakini tuna wajibu wa kuwawezesha vijana kuyafikia masoko makubwa kama ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC”.
Amesema CBE ina dhamana ya kuwapa maarifa wafanyabiashara nchini kuhusu namna bora ya kushiriki kwenye biashara ya kimataifa kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ya muda mfupi.
“Ni imani yangu kuwa bodi hii mpya itakuwa na jicho la kuangalia fursa mbalimbali za biashara za kufanya nchi iweze kusonga mbele, jitahidini kutengeneza Watanzania mahiri wenye uwezo wa kutumia fursa hizi za masoko,” amesema Waziri Jafo.
Aidha, ameipongeza CBE kwa kufanikiwa kuwapa mafunzo ya biashara wafanyabiashara wadogowadogo zaidi ya 2,000 namna bora ya kufanya biashara na amekitaka kuandaa mafunzo kwa wafanyabiashara wengine ili kuwaongezea maarifa ya biashara.
“Andaeni programu za muda mfupi kuhusu masuala ya uongozi, namna ya kufanya usaili wa kazi, kuandika barua ya kuomba kazi kwa wiki moja au mbili mkawapa watu maarifa ya kuwa mahiri kwenye sekta ya biashara, najua mnatoa mafunzo mengi lakini ongezeni kwasababu watu wanataka maarifa ya biashara,” amesema
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesema chuo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa kufanya tafiti mbalimbali za maboresho ya biashara.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga ameipongeza bodi iliyopita kutokana na mafanikio makubwa iliyopata katika kipindi cha uongozi wake kuanzia mwaka 2021-2024 ikiwamo kutengeneza dira ya miaka 50 ya chuo hicho inayoanzia 2025 mpaka 2075.
Amesema bodi iliyomaliza muda wake imefanikiwa kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi kwani ilipoanza mwaka 2021 kulikuwa na wanafunzi 10,034 lakini mpaka inamaliza muda wake ilifanikiwa kuongeza wanafunzi hadi 22,263 karibu nusu ya wanafunzi waliowakuta.
Amesema bodi hiyo imekiwezesha chuo kupanua programu zake kutoka Astashahada hadi Shahada za Uzamili na kufikia programu 63, na pia kutoa Shahada za Umahiri (online masters program) ambazo zimesaidia wanafunzi kusoma bila kuhudhuria darasani.
Amesema bodi pia imefanikiwa kuanzishwa kwa programu ya Shahada ya Uzamivu katika biashara ya infomatiki ambapo wadau mbalimbali wameshirikishwa kutoa maoni yao kwaajili ya kuiboresha na kupata ithibati ya kuanza kutumika.
Amesema wamefanikisha pia kuboresha miundombinu ya chuo hicho ambapo mwaka 2023 walianza ujenzi jengo la metrolojia wa ghorofa 10 utakaogharimu Shilingi bilioni 22.4 ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Zacharia Mganilwa amesema anafahamu kuwa ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi wanahitajika wataalamu wenye ujuzi na maarifa hivyo utakuwa wajibu wa chuo kuhakikisha wataalamu hao wanapatikana.