WAHITIMU wa kidato cha nne nchini wametakiwa kuacha mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha badala yake watumie rasilimali za nchi kuongeza pato la Taifa.
Hayo yamesemwa Jijini na Mkurugenzi Mtendaji wa (SUMA JKT) Brigedia Jenerali Petro Ngata wakati wa mahafali ya 40 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Jitegemee JKT.
Ngata amesema baadhi ya vijana wamekuwa na mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha mazuri na kuacha rasilimali zilizopo ambazo mataifa ya nje wanazifuata.
“Msitamani kwenda majuu kwani wa huko wanatamani kuja huku kutumia rasilimali zetu ambazo Mungu ametubariki kuwa nazo na hazipo kokote kule zaidi ya Tanzania hivyo tumieni maarifa mliyopata ili kuzitumia,”amesema Ngata.
Aidha amesema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo na kuacha kushiriki kwenye mambo maovu hasa yale yanayohamasishwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo siasa uchwara na kuwa na nidhamu nakutojiingiza kwenye masuala ya ngono.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Kanali Robert Kesi amesema kuwa wamewaandaa vizuri wanafunzi kwa kufanya mitihani mingi ya majaribio yenye hadhi ya kitaifa kwa nadharia na vitendo na wameiva.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Shule Bregadia Mstaafu Lawrence Magere amesema kuwa wanategemea changamoto zilizopo shuleni hapo zitafanyiwa kazi na wanawapongeza walimu kwa maandalizi mazuri kwa wanafunzi hao.
Awali akisoma risala ya wahitimu Shekha Said amesema kuwa moja ya mafanikio waliyopata ni kujifunza elimu ya ujasirismali ambapo wanaweza kutengeneza sabuni, kilimo cha mbogamboga, kutengeneza balbu zilizoungua na kurudi kufanya kazi kama zamani jumla ya wahitimu 89 waliagwa shuleni hapo.