Latest Posts

KUKOPA SI AIBU, NI AFYA KIUCHUMI: WAZIRI SIMBACHAWENE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema mikopo ni moja ya vyanzo vya mapato ya serikali kote duniani hivyo Tanzania kukopa siyo aibu wala kujidhalilisha bali ni sifa njema kwa kuwa inakopesheka.

Simbachawene ametoa kauli wakati akizungumza kwenye harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kubadilisha paa la Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu, Yuda Tadei Mang’ola Chini, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha ambalo limekuwa likivuja wakati wa mvua na hivyo kusababisha wakristo kushindwa kukaa ndani.

Amesema vyanzo vya mapato vya kanisa ni pamoja na sadaka ya kila Jumapili, zaka, misaada mbalimbali na harambee huku akitaja vyanzo vya mapato vya Serikali kuwa ni kodi, tozo, misaada na mkopo.

“Vyanzo vya mapato vya Kanisa ni sadaka ya kila jumapili, zaka, misaada mbalimbali pamoja na harambee ambapo harambee ni hatua ya mwisho ya utafutaji wa fedha kwa Taasisi za dini, lakini vyanzo vya mapato vya Serikali ni kodi, tozo, misaada na mkopo, hivyo kukopa ni moja ya chanzo cha mapato ya serikali na serikali zote duniani zinakopa” Amesema Simbachawene.

Aidha amesema kama ingetokea Tanzania haiwezi kukopesheka hiyo ndiyo ingekuwa aibu lakini kwa kuwa inakopesheka ni heshima kubwa kwa Watanzania kwa kuwa inakopa ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwani kodi inayokusanywa nchini haina uwezo wa kutekeleza miradi hiyo na kama kodi hiyo itaweza kutumika inaweza kuchukua zaidi ya miaka 40 ili kukamilisha miradi hiyo.

“Kukopa ni chanzo cha mapato hivyo isionekane Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapokwenda kutafuta mkopo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo ndiyo inakopa sana” Ameeleza Simbachawene.

Amesema kutokana na mahitaji makubwa ya nchi suala la kukopa haliepukiki akitolea mfano uendelezaji wa Bwawa la Kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambalo gharama yake ni zaidi ya trilioni 6 huku bajeti ya Serikali ya mwaka mzima ikiwa ni trilioni 43 huku zaidi ya asilimia 7O ya fedha hizo zikitumika kwa ajili ya uendeshaji wa nchi na asilimia 30 ndizo hupelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hata hivyo Simbachawene amesema kwa mujibu wa kanuni za fedha duniani zinaipa Tanzania wigo wa ukomo wa kukopa na kama nchi bado ina sifa ya kukopa kwa sababu bado haijafikia kikomo hicho.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!