Na Helena Magabe -Tarime.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini, Petro Ntogoro, amesema kuwa Madiwani wanayo mamlaka ya kuwaagiza na kuwasimamia watumishi kutekeleza miradi ya maendeleo, bila kusubiri kauli kutoka kwa Mkuu wa Mkoa.
Kauli hiyo ameitoa wakati akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri, alipokuwa akijibu hoja za baadhi ya Madiwani waliolalamikia kutotekelezwa kwa miradi ya barabara, wakidai hali hiyo inasubiri uamuzi kutoka ngazi ya Mkoa kama ilivyokuwa kwa mradi wa madawati uliofanikishwa kwa msaada wa CSR.
“Mkuu wa Mkoa huingilia pale tu ambapo tumeishiwa mbinu. Madiwani tuna mamlaka ya kusimamia miradi. Baraza hili ni mahali pa kutoa maamuzi, tusisubiri kila jambo lishikwe juu,” alisema Ntogoro.
Barabara Zina Kero Kubwa, Kata Zatelekezwa
Akizungumza kwa uchungu kuhusu hali ya miundombinu, Ntogoro alisema kuwa barabara nyingi zimeharibika kutokana na mvua, na katika kata yake ya Mwema, barabara zilizofanyiwa kazi zimejaa udongo badala ya kufanikisha upatikanaji.
“Kero ya barabara ni kubwa sana. Kata 12 bado hazijafikiwa na miradi. Tunahitaji hatua za haraka kabla ya uchaguzi mkuu,” alisisitiza.
Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara, ambaye pia ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, aliongeza kuwa kuna miradi yenye bajeti kubwa lakini utekelezaji wake ni duni – akitaja mradi wa barabara wa Sh milioni 600 uliotokana na mapato ya ndani na fedha za CSR ambao haujatekelezwa ipasavyo.
“Kuna barabara kama ya kijiji cha Nyamurege, iliyotengewa milioni 37 tangu 2023/24, lakini hadi leo haijawekwa hata kifusi,” alisema Sagara.
Alienda mbali zaidi akidai mkandarasi anayehusika na mradi huo amekuwa akitoa taarifa za uongo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri Solomon Shati, Mhandisi Robina Katushabe, na yeye binafsi.
Madiwani Wahoji Mgawo wa Miradi
Malalamiko mengine kutoka kwa Madiwani wa Kata za Gorong’a, Nyarukoba, Nyarero na Binagi yaliibua sintofahamu kuhusu ugawaji wa fedha hizo za miradi. Diwani wa Binagi, Marwa Marigiri, alihoji kwa nini kipande cha barabara katika kata yake kimetelekezwa licha ya kupakana na kata ya mjini ya Kitale.
“Kama kata yangu haimo kwenye mgawo wa milioni 600, basi naombeni majibu rasmi,” alisema Marigiri.
TARURA: Kazi Itaanza Baada ya Mvua Kukoma
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa, alikiri kuwepo kwa changamoto lakini aliahidi kuwa kazi zitaanza mara mvua zitakapokoma.
“Tumeshafanya kazi kubwa mwaka wa fedha uliopita. Kwa mwaka huu wa fedha 2024/25, mikataba ya mradi wa Sh milioni 600 imeshasainiwa, kazi zitaanza muda si mrefu,” alisema Marwa.
Alifafanua kuwa hadi sasa kata 16 kati ya 26 zimefikiwa, barabara mpya zimezibuliwa katika kata 10, ukarabati umefanyika katika kata 4, na TARURA imepanga kufanikisha kazi kwenye kata 12 zilizosalia kabla ya mwaka wa fedha kumalizika.