Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa mwezi mmoja kwa wamiliki na waendeshaji wa pikipiki za mizigo zinazotumia umeme maarufu kama maguta, kuhakikisha wanasajili vyombo hivyo rasmi, kuwa na leseni za udereva na za usafirishaji kutoka LATRA pamoja na bima halali.
Mpogolo ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati wa kikao kilichowakutanisha wamiliki na madereva wa vyombo hivyo jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa maguta hayo yameongezeka kwa kasi maeneo ya katikati ya jiji, huku mengi yakiwa hayana usajili, bima wala leseni za udereva, jambo linalohatarisha usalama wa raia na kusababisha kero kwa wafanyabiashara.
“Ninatoa mwezi mmoja kuanzia sasa pikipiki zote zinazotumia umeme (maguta) zisajiliwe rasmi. Pia ziwe na leseni kutoka LATRA, ziwe na bima na madereva wote wawe na leseni za udereva,” amesema Mpogolo.
Amesisitiza kuwa lengo ni kurasimisha usafiri wa maguta, kama ilivyo kwa bodaboda na bajaji, kuhakikisha madereva na vyombo vyao wanalindwa kisheria ikiwemo kupata fidia ya bima pale wanapopata ajali.
Pia amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha linapima ubora wa vyombo hivyo kabla ya kuingia barabarani.
Katika kuleta urahisi wa utekelezaji wa agizo hilo, Mpogolo ametangaza kuwa kutakuwa na kituo maalum cha pamoja cha usajili, kitakachojumuisha Halmashauri ya Jiji, LATRA, makampuni ya bima na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kurahisisha mchakato wa usajili na utoaji wa elimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema hatua hiyo inalenga kuweka mazingira bora ya biashara kwa wamiliki wa maguta, huku akiwasihi wafuate sheria na kushirikiana na serikali.
“Tutakuwa nanyi bega kwa bega. Lakini tunasisitiza tufanye biashara kwa kufuata utaratibu na sheria bila bughudha ya aina yoyote,” amesema Mabelya.
Baadhi ya madereva waliohudhuria mkutano huo wameunga mkono agizo hilo lakini wakaomba muda zaidi.
“Utaratibu ni mzuri lakini tunaomba muda zaidi kwa sababu mwezi mmoja hautoshi kukamilisha kila kitu,” amesema dereva mmoja, Omary Awadhi.
Wananchi wa maeneo ya katikati ya jiji pia wamepongeza hatua hiyo wakieleza kuwa maguta yamekuwa kero kutokana na kuendeshwa kiholela, bila usajili wala kufuata sheria za usalama barabarani.