
Na Amani Hamisi Mjege.
Katika miaka ya hivi karibuni, huduma za usafiri wa taxi mtandao zimebadilisha kwa kiasi kikubwa jinsi Watanzania wanavyosafiri, huku kampuni kama Uber na Bolt zikiongoza njia katika sekta hii. Hata hivyo, nyuma ya urahisi wa matumizi ya teknolojia kwa wateja, kuna mgogoro ambao umekuwa ukija na kuondoka mara kadhaa.
Hauwezi kuutaja mgogoro huu pasina kuwahusisha wadau wakubwa kwenye sekta hii ambao ni madereva wa taxi mtandao, kampuni zinazotoa huduma hizo, na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA). Madereva wa taxi mtandao wamedai kuwa wamekuwa wakipambana na changamoto nyingi, zikiwamo makato makubwa na bei ambazo wanadai zinakiuka taratibu zilizowekwa na LATRA, huku wakihisi kutotetewa ipasavyo na Umoja wa Madereva wa Mtandao Tanzania (TODA).
Mmoja wa madereva wa taxi mtandao, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu za kiusalama, ameeleza jinsi hali ya sasa inavyowaathiri wao kama madereva.
“Changamoto ambazo zinatukumba sisi madereva ni upunguaji wa bei kwa kila kilomita. LATRA ilipanga bei maalumu mwaka 2022, lakini kampuni za taxi mtandao zinakiuka taratibu hizo kwa kushindana kushusha bei,” amesema dereva huyo, akiongeza kuwa,
“Sasa inapotokea kundi la watu na kampuni ambazo unafanya nazo kazi kwenda kutukandamiza, ni hatari kwa maisha yetu. Bei zilizopangwa kwa kilomita kwa magari, bajaji, na bodaboda zimekiukwa. Kwa mfano, kwa kila safari, LATRA ilipanga kwamba madereva wa magari wanatakiwa kukatwa 15% tu lakini sasa tunakatwa hadi 25%,”
Madereva hawa wanasema kuwa, licha ya juhudi zao za kila siku, hawawezi tena kumudu gharama za maisha kutokana na makato hayo makubwa na bei ndogo wanazopokea kwa safari wanazofanya.
“Tuna familia, tuna majukumu, na tunategemea kazi hii ya taxi mtandao kuweza kupata riziki. Lakini kampuni zinazotuajiri zinatudhulumu kwa kutushusha bei, huku gharama zetu za uendeshaji, kama vile mafuta na mtandao, zikiwa juu sana,” ameongeza dereva huyo kwa huzuni.
Pamoja na changamoto za kiuchumi, madereva wengi wanaonekana kutokuwa na imani na chama kinachowawakilisha, TODA.
“Chama hiki hakitusaidii kwa lolote. Tumekuwa tukihisi kwamba viongozi wetu wamepewa rushwa na kampuni za usafirishaji ili kukaa kimya na kutotetea maslahi yetu,” amesema dereva mwingine wa taxi mtandao.
Madereva wengi wanahisi kuwa sauti zao hazisikilizwi, na hawapati mwongozo wowote kutoka kwa chama chao.
“Changamoto ni nyingi, nauli zipo chini kiasi kwamba safari niliyofanya juzi kutoka Makumbusho kwenda Salasala kwa bajaji ililipwa Shilingi 6,500 tu. Hii ni bei ndogo sana ukilinganisha na bei ya mafuta ya sasa. Tumefikia hatua ya kutamani kukata tamaa,” amesema dereva huyo.
Jambo TV imemtafuta Katibu Mkuu wa TODA, Ebony Ford, ambaye ameeleza kuwa licha ya changamoto ambazo madereva wamezibainisha, wanapaswa kutambua juhudi zinazofanywa na chama hicho katika kutetea maslahi ya madereva wa taxi mtandao, huku akikanusha na wao kupokea hongo ya aina yoyote.
“Mwaka 2022, LATRA ilipanga bei maalumu ya Shilingi 1,000 kwa kila kilomita ya gari na asilimia 15 ya makato kwa kila safari. Tuliona haya kama mafanikio makubwa kwa madereva,” amesema Ford. Hata hivyo, Ford amekiri kuwa ushindani kati ya kampuni za usafirishaji umesababisha kushuka kwa bei na kuongezeka kwa makato, jambo ambalo limeathiri maisha ya madereva.
Kwa upande wake, TODA inasema imekuwa ikipambana kuhakikisha madereva wanapata mazingira bora ya kazi.
“Tunawasiliana na LATRA mara kwa mara kuhusu changamoto hizi. Tarehe 16 Oktoba 2024, tumealikwa kwenye kikao cha pamoja na LATRA ili tujadili changamoto zinazowakabili madereva, na tumewaalika madereva watano ambao siyo wanachama wa TODA kuhudhuria,” ameongeza Ford, akisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua matatizo haya ni kwa kufanya kazi kwa pamoja, licha ya baadhi ya madereva hao kutaka kujitenga katika mkutano huo na LATRA.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa upande wake, imekuwa ikijaribu kusawazisha hali ya mambo. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, ameeleza kuwa madereva wenyewe walikuwa na mchango mkubwa katika kuleta hali hii.
“Madereva wa taxi mtandao ndio waliosababisha Uber na Bolt kusitisha huduma zao nchini mwanzoni. Baada ya muda, haohao madereva walikuja kutuomba turuhusu kampuni hizo zirejee, kwani kampuni za ndani hazikuwa na wateja wa kutosha,” amesema Pazzy.
Pazzy amefafanua kuwa LATRA imeweka mfumo wa ushindani wa bei ili kuwapa madereva uhuru wa kuchagua kampuni inayowafaa.
“kupitia maoni hayohayo ya wadau kuwa suala la commission libaki huria yaani mtu au dereva ambaye akiona commission ya kampuni A ni kubwa aende kwenye kampuni B, ambapo kampuni nyingi za Dar es Salaam zilikubali kukata commission ya asilimia 15, kwahiyo amri ya mwisho ambayo LATRA tuliitoa inaruhusu ushindani kwenye commission, tumeweka bei ya ukomo ya juu na ya chini ili kumlinda mtumiaji huduma na kumlinda dereva,” ameongeza Pazzy.
Hata hivyo, LATRA imeeleza kuwa mchakato wa marejeo ya nauli unahusisha maoni ya wadau, na serikali haiwezi kubadilisha bei au makato bila ushirikishwaji. “Mchakato wa kubadili bei unahitaji mijadala na maoni ya wadau wote, hatuwezi kubadilisha bila makubaliano ya pamoja,” amesema Pazzy, akiwataka madereva kushiriki kwenye mikutano ili kutoa maoni yao.
Mgogoro huu kati ya madereva wa taxi mtandao, kampuni za usafirishaji, na LATRA unaonesha ugumu wa kusawazisha maslahi ya pande zote. Wakati madereva wakilia kwa makato makubwa na bei za chini, kampuni za usafirishaji zinadai kuwa hali ya soko na ushindani inawalazimu kuchukua hatua hizo ili kubaki kwenye biashara. Wakati huo huo, LATRA inajaribu kusawazisha maslahi ya wadau wote kupitia mfumo wa ushindani.
Ikiwa hakuna suluhisho la haraka linalopatikana, inawezekana mgogoro huu utaendelea kudhoofisha sekta ya usafirishaji mtandao nchini Tanzania, hali ambayo inaweza kuathiri zaidi maisha ya madereva wanaotegemea kazi hii kama chanzo kikuu cha mapato yao. Madereva hawa wamesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuzima program tumizi za kampuni za usafirishaji mtandao kushinikiza masilahi hayo, ikiwa hili litatokea huenda si tu wao wataathiriwa, bali pia wateja na wale wote walio katika sekta hiyo muhimu ya uchumi nchini.